Polo aliyedhani ndoa ni asali tu ajua ukweli

Na CORNELIUS MUTISYA

Imepakiwa - Sunday, June 12  2016 at  14:56

Kwa Muhtasari

KAVIANI, Machakos

Polo wa eneo hili alijipata pabaya alipokataa kuwajibikia mimba aliyompachika mwanadada akisema alikuwa akisingiziwa.

 

POLO wa eneo hili alijipata pabaya alipokataa kuwajibikia mimba aliyompachika mwanadada akisema alikuwa akisingiziwa. Hata hivyo, mtoto alipozaliwa na wakapimwa chembechembe za DNA, iligunduliwa alikuwa mtoto wake halisi.


Penyenye zinaarifu kuwa polo alianza uhusiano wa kimapenzi na mwanamke huyo ambao ulinoga hadi demu akahamia kwa polo katika ndoa ya 'njoo tuishi’.


“Polo na demu walikuwa wakiishi pamoja kama mume na mke. Hata hivyo, hawakuwa wamefuata utaratibu unaotakiwa kulingana na mila na desturi za jamii ya hapa,’’ akasema mdokezi.


Inasemekana demu aliishi na jamaa huyo kwa muda wa miezi minane na akabeba mimba yake. Alipomwambia polo kuhusu mimba hiyo, alikasirika na akamfurusha kinyama.


“Jombi aliposikia kuwa demu alikuwa mja mzito, alikasirika na kufoka kuwa mimba haikuwa yake. Alimwamuru kufunganya virago vyake na kutokomea,’’ akasema mdokezi.


Inasemekana kwamba jitihada za demu kumtuliza polo zilipoambulia patupu, aliamua kwenda kuripoti kisa hicho kwa naibu wa chifu ili suluhisho lipatakane.


Duru zinaarifu kwamba chifu aliposikiliza madai ya demu huyo, alimshutumu kwa kuamua kuishi na polo huyo kana kwamba alikuwa amemuoa. Alimwambia ikiwa alikuwa na hakika mimba ilikuwa ya polo huyo, basi asubiri mtoto atakapozaliwa wapimwe damu ili ukweli udhihirike.


Na mtoto alipozaliwa na wote wakapimwa, ilidhihirika bayana kuwa alikuwa wa polo huyo. Walienda kwa naibu wa chifu na polo akaamriwa agharamie malezi na elimu ya mtoto wake hadi atakapotimu umri wa miaka 18.


“Polo alikubali kugharamia mahitaji ya mtoto huyo, lakini alikataa katakata shinikizo za wazazi wake kumuoa mwanadada huyo,’’ akasema mdokezi.