Mke ala makonde kwa kufagia minofu ya nguruwe peke yake

Imepakiwa Sunday August 7 2016 | Na TOBBIE WEKESA

Kwa Muhtasari:

Jombi aliwaacha wenyeji wa eneo hili vinywa wazi baada ya kumpa mkewe kichapo kikali akidai alimmalizia kitoweo cha nyama ya nguruwe.

JOMBI aliwaacha wenyeji wa eneo hili vinywa wazi baada ya kumpa mkewe kichapo kikali akidai alimmalizia kitoweo cha nyama ya nguruwe.


Yasemekana polo alinunua nyama ya nguruwe kilo moja na mkewe akaamua kuipika yote japo mumewe hakutaka nyama hiyo ipikwe yote.
“Mbona umepika nyama yote? Si ungebakisha nusu ili ipikwe kesho,” polo alifoka. Penyenye zinasema kuwa kipusa alimueleza polo kuwa hawangekula yote.


“Wewe usijali. Hii nyama ni nyingi sana. Tutabakisha nyingine itumike kesho,” mke huyo alimueleza polo. Inasemekana kuwa polo alikubaliana na mke lakini kwa shingo upande.


Duru zinaarifu kuwa kulipopambazuka, polo alienda shughuli zake za kila siku huku akimuacha mkewe nyumbani. Inasemekana kuwa mchana mke huyo alitayarisha chakula na kukila kwa nyama iliyosalia jioni ile kama kitoweo. 


Lakini kwa bahati mbaya, yamkini kutokana na utamu wake, mke akaufagia mnofu mzima bila kubakisha. Jamaa aliporejea kwake kwa hamu ya kufakamia kitoweo chake cha nguruwe, alishtuka.


“Jamaa hakuamini macho yake alipoandaliwa ugali kwa mboga za kienyeji,” alieleza mdokezi. Inasemekana kuwa polo alichungulia tena kwenye sahani ili kuthibitisha alichoona.


“Nguruwe ya jana kwani umesahau kuleta?” polo aliuliza. Duru zinasema kuwa mkewe alimueleza kuwa nyama ya nguruwe iliisha.
“Wewe ukiondoka asubuhi, uliniachia pesa za mboga kweli? Nilipika ugali mchana nikala na hiyo nguruwe,” kipusa alimueleza polo.
Duru zinasema kuwa polo aliinuka na kuanza kumzaba mkewe makofi kwa hasira.


“Mimi sikuoa mke mlafi. Unawezaje kula nusu kilo ya nyama ya nguruwe peke yako?” polo alimuuliza kipusa huku akiendelea kumpa makofi.
Inasemekana kuwa majirani walishangazwa na sababu ya polo kumchapa mkewe.

Share Bookmark Print

Rating