Kalameni ajuta kurina asali ya bawabu

Na KIMANI wa NJUGUNA

Imepakiwa - Friday, August 12  2016 at  19:45

Kwa Muhtasari

GITAMBAYA, Ruiru

Kalameni wa hapa alijipata pabaya alipofumaniwa akichovya asali kutoka mzinga wa jirani yake ambaye ni bawabu.

 

POLO wa hapa alijipata pabaya alipofumaniwa akichovya asali kutoka mzinga wa jirani yake ambaye ni bawabu.
Habari zilizotufikia zasema kwamba jirani huyo hufanya kazi usiku na kurejea kwake asubuhi na mkewe hufanya vibarua mitaani.

Inasemekana kuwa polo mhusika alimaliza kidato cha nne mwaka uliopita. “Polo hutegemea vibarua vya hapa na pale ili kujikimu kimaisha na kwenye harakati za kutafuta vibarua, alikutana na mke wa bawabu mwenye sura na umbo la kupendeza,” alisema mdokezi.

Wawili hao walifanya urafiki ambao uliota mizizi na akaanza kumtembelea mama huyo jioni. Isitoshe, mara kwa mara alikesha nyumbani kwa mama huyo wakila fuska kwani mwanamke huyo alidai alihitaji mtu wa kumkinga na baridi usiku!

Wawili hao hawakuwa na bahati kwa sababu mwenye mzinga alipashwa habari kuhusu uhusiano wao na wadaku wa mtaa.

Siku arobaini za walaghai hao wa mapenzi zilipotimia, hawakuweza kuepuka. Siku hiyo, bawabu aliamua kuacha kazi yake na kurejea nyumbani usiku wa manane. Badala ya kubisha mlango, aliuvunja kwa kishindo na kujitoma ndani ya chumba cha kulala alipowafumania wakiwa kitandani uchi wa mnyama.

“Nyinyi kweli mna akili timamu? Kijana, ikiwa hujui siku za kuchovya asali katika kila mzinga zilipita na wakati huu ni hatari, basi nitakufunza leo,” alifoka mzee na kuanza kumtwanga jamaa kwa rungu yake.

Vurugu hizo ziliwavutia majirani ambao walifika kujua kilichokuwa kikiendelea. Ni wakati huo ambapo polo alipata mwanya na kufyatuka kama mshale akiwa uchi.

Ajabu ni kwamba bawabu hakusema lolote kwa mkewe kuhusu kitendo hicho.