Kipusa amgeuka pasta mumewe siku ya harusi

Na BENSON MATHEKA

Imepakiwa - Tuesday, August 23  2016 at  16:37

Kwa Muhtasari

EMBAKASI, Nairobi

KIOJA kilitokea hapa demu alipokataa kufunga harusi baada ya kugundua kwamba mchumba wake ambaye ni pasta alikuwa na mpenzi mwingine.

 

Wiki moja kabla ya siku ya harusi, mwanadada huyo alichukua simu ya mkewe akitaka kuwasiliana na kamati ya harusi kwa sababu hakuwa na mjazo katika simu yake.

Ni katika harakati za kuwaandikia wanakamati arafa alipopata jumbe ambazo mumewe alitumiwa na mama mmoja aliyemfahamu akimpongeza kwa mapenzi yake motomoto.

“Aliposoma arafa hizo, mwanadada huyo alikasirika hadi akashindwa kupumua. Alimwendea mumewe aliyekuwa chumba cha kulala na kumuuliza kwa nini alikuwa na wachumba wengine ilhali walikuwa wanakaribia kufanya harusi,” alieleza mdokezi.

Inasemekana kuwa maandalizi yote yalikuwa yamekamilika na mwanadada huyo alijipata amechanganyikiwa.

“Badala ya jamaa kuomba msamaha, alimwambia kipusa aamue ikiwa wataendelea na mipango ya harusi au la.

Lilikuwa tamko lililozidisha uchungu katika moyo wa mwanadada huyo. Alishindwa kulala kwa sababu ya mawazo na siku iliyofuata aliamua kusitisha harusi,” akasema mdokezi.

Kulingana na msimulizi wetu, mipango ya harusi ilipokuwa ikiendelea, jamaa alikuwa amepagawisha kimapenzi na mwanadada mwingine tajiri aliyemzidi kwa umri.

“Baada ya harusi kusitishwa jamaa alinyakuliwa na mama sukari huyo huku wakazi wakimsimanga mwanadada kwa kuwahadaa alikuwa na harusi ili wamchangie pesa. Mwanadada huyo alikosa amani, ikawa vigumu kufanya lolote kwa sababu ya masaibu yanayomwandama,” alisema mdokezi.

Demu alipowaeleza wazazi wake sababu za kusitisha harusi walikubali uamuzi wake lakini wakawa na wakati mgumu kuwaeleza watu walioalika kushuhudia binti yao akifunga pingu za maisha.

“Kwa sasa demu anatafuta mchumba, huku jamaa akiendelea kupata joto kutoka kwa mama sukari,” akasema mdokezi.