King'asti msomi atimuliwa kwa kuposwa na taniboi

Na KIMANI NJUGUNA

Imepakiwa - Wednesday, August 24  2016 at  17:21

Kwa Muhtasari

THARAKA-NITHI, Meru

KIPUSA mmoja kutoka hapa alilazimika kutoroka kwao baada ya wazazi wake kumkataa mpenzi wake walipogundua kwamba alikuwa makanga wa matatu.

 

Yasemekana kuwa msichana huyo alimaliza chuo kikuu miaka mitatu iliyopita. “Bahati iliendelea kumfuata msichana huyo kwani mara tu alipofuzu kutoka chuo kikuu, aliajiriwa na kampuni moja ya kibinafsi mjini Nairobi,” akasema mdokezi.

Ni akiwa kazini katika kampuni hiyo ambapo alijuana na kupendana na kijana mmoja makanga wa matatu. “Wawili hao walipendana sana. Hata hivyo, kwa sababu msichana huyo ni Mkristo aliyeokoka, waliamua kutofanya mapenzi kabla ya kufunga ndoa.

Ni kwa sababu hiyo wawili hao waliamua kwenda nyumbani kwa kina msichana huyo ili wawaeleze wazazi wake kuhusu uamuzi huo wa kuoana.

Walipowasili, walipokelewa vizuri na wazazi wakidhani jamaa alikuwa mshiriki wa kanisa lao. Mambo yalipasuka mara tu jamaa alipoeleza kilichomleta na kazi anayofanya.

“Ati nini? Wewe makanga umuoe binti yangu ambaye nimesomesha hadi chuo kikuu ili awe fahari kwa familia yetu. Nikubali binti yangu aolewe na makanga wa matatu? Wewe kijana unataka kumpotosha binti yangu na sitakubali kamwe,” mzee alifoka.

Mzee huyo alijitoma ndani ya nyumba na kuchomoka amebeba rungu mkononi. Bila kujali alimkaribia jamaa huyo aliyechomoka kama mshale ili kujinusuru.

Kuona hivyo, msichana alichomoka na kumfuata mapenzi wake huku akilia kwa sauti ya juu. Kulingana na mdokezi, msichana huyo aliapa kutorejea kwa wazazi wake hadi wamruhusu kuolewa na barafu ya moyo wake.

Haikujulikana iwapo mzee alibadilisha nia na kukubali wapenzi hao kuoana.