Buda na kipusa wazua sinema ya bure kwa baa

Na TOBBIE WEKESA

Imepakiwa - Thursday, August 25  2016 at  11:12

Kwa Muhtasari

MWIHOKO, GITHURAI 45

KIOJA kilizuka katika baa moja inayopatikana eneo hili baada ya polo na kipusa kuraruliana nguo hadharani wakizozania bili ya pombe.

 

Inasemekana kuwa wawili hao walikabana koo baada ya kutofautiana kuhusu nani alifaa kulipa bili ya vinywaji walivyokunywa.

Kulingana na mdokezi, polo na kipusa waliingia katika baa pamoja. Inasemekana kuwa polo alimwambia kipusa kuitisha aina ya pombe anayopenda. Duru zinasema kuwa polo naye aliitisha kinywaji chake.

Inasemekana kuwa kadri muda ulivyozidi kusonga, ndivyo walivyozidi kuitisha kileo. Kulingana na mdokezi, meza yao ilikuwa imejaa vileo.

Penyenye zinasema kuwa muuzaji alipogundua kuwa polo na kipusa walikuwa wamelewa, aliwaendea na kuitisha pesa, naye polo alimueleza atulie kidogo.

Duru zinasema kuwa ulifika wakati kipusa alitaka kuondok na kulingana na mdokezi, polo alimueleza kipusa alipe nusu ya bili naye alipe nusu. “Ni wewe ulinileta hapa. Kwa hivyo lipa bili,” kipusa alimkaripia polo. Inasemekana kuwa polo aliingiza mikono mifukoni na kuchomoa Sh100 peke yake.

“Unaniambia nikulipie bili ni kama ni mimi nilikunywa hizi chupa zote. Leo sina pesa. Kila wakati ni mimi nakulipia. Hata na wewe lipa leo. Sio kunikamua tu kama ng’ombe,” polo alimueleza kipusa.

Duru zinasema kuwa kipusa aliinuka na kumshika polo shati kwenye shingo. “Sikia, ujinga ndio sitaki,” kipusa alimsomea polo

Kulingana na walioshuhudia kisa hiki, polo alimkaba koo kipusa na wakaanza kurushiana makonde. “Kama unajua umesota, why call me here?” kipusa alimuuliza polo. Iibidi muuzaji wa baa hiyo kutisha kuwaita polisi ndipo jamaa akalipa bili.