Jombi amtoroka 'mpango wa kando' ndotoni uchi

Na TONY NYONGESI

Imepakiwa - Sunday, September 4  2016 at  18:37

Kwa Muhtasari

KANGEMI, Nairobi

WAKAZI wa hapa walishabikia kisa cha kushangaza jombi alipochomoka nyumbani uchi wa mnyama akiwa kwenye ndoto akidai alikuwa akikimbizwa na mpango wa kando.

 

Jamaa ambaye huchapa vinywaji wikendi  aliamua kulala mapema ili kuepuka kuchelewa kazini kumbe alikuwa akialika mkosi uliomweka mashakani.

Ilipotimia saa tatu usiku, jombi ambaye kawaida  hulala bila mavazi aliangua kilio usingizini akitaja jina la mpango wa kando.

“Wewe  unanihangaisha kwa nini na nilikuwa nimekulipa? Mbona wataka kunikatakata Jessi na nimegharamia kila kitu?” alilia jombi kwa sauti ya juu akiwa usingizini.

Mkewe na wanawe waliokuwa wakiandaa chakula cha jioni, waliingiwa na wasi wasi na  ghafla bin vuu, jombi alichomoka kwenye chumba cha kulala na kutoka nje mbio akiangua kilio na kumtaka Jessi amwachilie.

“Wewe Jessi, ukiendelea hivi sitarudi hapa tena,” jombi alipiga kelele huku akitembea nje ya ploti. Ajabu ni kwamba wakati huu wote, kalameni alikuwa amevalia chupi bila shati wala kaptula ya kulala.

Kilio cha mkewe kilifuata  huku akitaka kumjua Jessi alikuwa nani.

Inasemekana kuwa mama alizuiwa kumhangaisha mumewe kwani alielezwa na baadhi ya watu kwamba si vyema kumsumbua mtu akitembea akiwa usingizini kwa sababu anaweza kunyakuliwa na mashetani.

Kulingana na mdokezi wetu, mzee alizunguka nje ya ploti na ajabu ya Musa, alirudi nyumbani na kujilaza kitandani huku akiendelea kukoroma.

Dakika chache baadaye aliamushwa na mkewe akitaka kujua Jessi alikuwa nani.

“Leo nimejua kimada wako ni Jessi na lazima utaniambia ni nani na alikufanyia nini. Sitaishi kwa hofu kila mara namna hii,” alichemka kwa hasira mama huku jombi akijitia hamnazo.