Landilodi mashakani kwa kutupa chambo plotini

Imepakiwa Wednesday March 15 2017 | Na JOHN MUSYOKI

Kwa Muhtasari:

NGETANI, Masinga

KIOJA kilitokea sehemu hii landilodi alipokabiliwa vikali na wapangaji na mkewe kwa tabia ya kunyemelea wake wa watu plotini.

Siku ya kioja, landilodi alipatikana katika chumba cha mwanamke mmoja mpangaji akimrushia mistari ya mapenzi. Hata hivyo, juhudi zake ziliambulia patupu mkewe alipofika kwenye ploti huku akibeba upanga na kufoka kwa ukali.
“Unafanya nini katika nyumba ya mwanamke.

Umekuwa kahaba? Leo umepatikana na lazima nikupe funzo,” mke wa jamaa alifoka na kuingia chumbani.
Wakati huo jamaa alijawa na hofu tele na kuanza kutetemeka ungedhani alikuwa ameugua maradhi ya kifafa.

Inasemekana mkewe alianza kuwakemea vikali. “Wewe ni mwanamke sampuli gani unamchukua mume wangu na kumfanya mumeo.

Nitawaonyesha kilichomtoa kanga manyoya,” mama alianza kumpokeza mwanamke kichapo huku jamaa akipata nafasi ya kuhepa.

Jamaa alipotoka nje, alipata mlango wa ploti ukiwa umefungwa kwa kufuli kubwa na baadhi ya wapangaji wakiwa wameshika fimbo nzito tayari kumkabili mwizi wa mapenzi.

Penyenye zinasema kati ya wapangaji hao alikuwemo mume wa mwanamke aliyekuwa alipokezwa kichapo chumbani.
Kwa hasira walimrukia na kuanza kumtandika jamaa kisanga ambacho kilivutia watu wengi akiwepo pasta.

Vita hivyo, vilizimwa baada ya Mtu wa Mungu kuingililia kati na kuwatenganisha. “Acheni kupigana nina ujumbe kwenu,” pasta alisema.

Ni katika hali hiyo pasta alipowahubiria na kuwaomba kudumisha amani. Hata hivyo, landilodi alipiga magoti mbele ya mtumishi wa Mungu huku akikiri makosa yake. Baadaye pasta aliwaombea wote na kuwaambia uzinifu ni dhambi.

Share Bookmark Print

Rating