Aanikwa hadharani na mpenzi wake wa zamani kwa kuwa ovyo kitandani

Imepakiwa Monday October 2 2017 | Na TOBBIE WEKESA

Kwa Muhtasari:

Suna, MIGORI

WENYEJI wa eneo hili, walibahatika kutazama sinema ya bure baada ya mrembo kumzomea vikali mchumba wake wa zamani.

Inasemekana mrembo alichukua hatua hiyo baada ya kugundua kwamba polo alikuwa akimchafulia jina kijijini.
Kulingana na mdokezi, kabla ya wawili hawa kukosana, mrembo na polo walikuwa wakijulikana kijiji kizima.

Inadaiwa kwamba baada ya kuachana, mrembo alianza kusikia hadithi mbaya mbaya zikisambaa kijijini kumhusu.

Kulingana na mrembo, baadhi ya hadithi hizo zilikuwa ni habari ambazo walikuwa wamesikilizana na polo ziwe siri yao.
Penyenye zinasema mrembo alianza kufanya uchunguzi kubaini zilikotoka habari hizo. Inasemekana muda mrefu haukupita kabla ya mrembo kugundua kwamba mdaku alikuwa mchumba wake wa zamani.

Duru zinasema mrembo alifululiza moja kwa moja hadi kwa polo. “Shida yako ni gani. Si mimi nilikataa mambo yako. Mbona unatembea ukiniharibia sifa,” kipusa alimkaripia polo.

Inadaiwa kuwa polo alibaki mdomo wazi. “Hadithi zote nimezipata. Tangu lini nikawa bure kitandani. Tulipokuwa wachumba ulikuwa ukirina asali kila wakati bila kulalamika.

Leo hii unatembeza habari kinyume. Kweli nyani haoni kundule,” mrembo alizidi kumzomea polo. Aliendelea kubaki kimya tu!.

“Huyu jamaa anatembea akidai eti mimi napenda kula sana. Ni lini nimekuja kwako ukaninunulia hata soda pekee? Nikome kabisa,” mrembo alimshtumu polo.

Inasemekana polo aliamua kuondoka ili kuepa aibu na kumuacha mrembo pale.

“Umesahau kuwa ni mimi nilikuacha. Sema ukweli. Ni wewe ulikuwa ovyo kitandani ndiposa nikaamua kutafuta mwingine,” mrembo alimzomea polo huku vicheko vikitawala angani.

Share Bookmark Print

Rating