Afurusha walevi kwa kumkosesha usingizi

Imepakiwa Thursday May 25 2017 | Na JOHN MUSYOKI

Kwa Muhtasari:

KISANGA kilizuka hapa mama alipovamia kilabu kimoja usiku na kuwatimua walevi akiwalaumu kwa kumkosesha usingizi kwa kelele.

Mama huyo alijitoma katika kilabu hicho akibeba rungu na kuwaagiza walevi kuondoka kwenda nyumbani akisema hangevumilia kelele zao.
Inasemekana kuwa mama anaishi karibu na kilabu hicho na kila mara alilalamikia kelele za mapolo walizokuwa wakipiga hasa usiku wa manane. Siku ya kioja mama aliamua kuwafunza adabu. Aliamka usiku na kujitoma kilabuni na kuwaangushia walevi kichapo kikali.

“Mapolo walipigwa na butwaa kuona mama akiwaangushia kichapo bila huruma hali iliyowafanya kutimua mbio na kuacha muhudumu wa kilabu hicho akikabiliana na mama huyo,” alisema mdokezi.

Penyenye zaeleza kuwa mama alipata kuwa hata mhudumu wa kilabu hicho alikuwa mlevi kupindukia. Baada ya walevi kutoroka, mama alimkemea mhudumu huyo na kumpa kichapo kikali na kumuacha na maumivu.

“Utakuwa ukifunga kilabu mapema. Hakuna haja ya kupigia watu kelele kiasi hiki hadi wanashindwa kupata usingizi. Kutoka leo ambia wateja wako wapunguze kelele na usipofanya hivyo nitawachukulia hatua kali,” mama alifokea mhudumu wa kilabu. Inasemekana mama huyo aliamuru mhudumu huyo kufunga kilabu mara moja na kuondoka.

“Jombi alifanya alivyoambiwa huku akisimamiwa na mama huyo. Baada ya kilabu kufungwa, mama alirudi kwake na kulala. Kuanzia siku hiyo kelele zilikoma kwa sababu wateja hawakuruhisiwa katika kilabu hicho baada ya saa tatu usiku,” alisema mdokezi.

Mama alisema alichotaka ni haki yake ya kupata usingizi.

Share Bookmark Print

Rating