http://www.swahilihub.com/image/view/-/1656142/medRes/367743/-/x4jjy8z/-/05satocouple.jpg

 

CHOCHEO: Ahadi zinazotolewa watu wakiwa walevi au wakifanya mapenzi hugeuka ahadi hewa

Wachumba

Wachumba wakiwa wamekumbatiana. Picha/MAKTABA 

Na BENSON MATHEKA

Imepakiwa - Wednesday, November 8  2017 at  11:26

Kwa Muhtasari

IKIWA unapanga ndoa au kukubali kuolewa kwa sababu ya kuahidiwa makuu na mpenzi wako, huenda ukajipata pabaya. Wataalamu wa mapenzi wanatahadharisha kwamba ahadi za uchumba huwa hewa na hazifai kutumiwa kama msingi wa ndoa. Wanasema wengi wanaokubali kuolewa baada ya kuahidiwa makuu hujuta.

 

“Ahadi zinazotolewa na watu wanapotafuta wachumba huwa sio rahisi kutimizwa. Wanaokubali kuolewa baada ya kuahidiwa makuu na wachumba wao mara nyingi hujipata majutoni,” asema mtaalamu wa mapenzi Jedna Moraa wa kituo cha Love Care, Nairobi.

Bi Moraa anasema idadi kubwa ya wanaume, huwaahidi makuu vipusa ili wakubali kuolewa jambo ambalo ni hatari.
“Ahadi zikikosa kutimizwa penzi haliwezi kudumu na nyingi ya ahadi huwa hewa tupu,” asema. Mtaalamu huyu anaongeza kwamba hii ni kwa sababu kinyume na awali ambapo watu walipendana bila kuwekeana masharti, siku hizi dunia imebadilika huku wengi wakiongozwa na tamaa.
“Watu wamekolewa na tamaa tu na imekuwa ni vigumu watu kufunga ndoa pasipo kuwekeana masharti na ahadi,” asema Bi Moraa. Anasema ingawa hatua hiyo inafaa wahusika wakiwa na nia njema, wanapaswa kuelewa kwamba inaweza kuathiri maisha yao ya ndoa siku za baadaye wakipatiana ahadi zisizoweza kutimilika kwa urahisi. Kulingana na Bw Isaac Miriti wa shirika la Life Love Circle, Nairobi, ahadi hizi huwapa wapenzi fursa ya kuelezea hisia zao na wakati mwingi zinaweza kufanyika katika mazingira yasiyofaa.
“Kwa mfano ahadi zinazofanywa watu wakiwa walevi au wakifanya mapenzi au kwa shinikizo huwa hazitimiliki,” asema. Mtaalamu huyu anasema watu wengi huamini kuwa ahadi hizi huongeza ladha ya huba.

“Nyakati ambazo wachumba walikubali kuoana bila masharti sasa zimepitwa na wakati. Masharti hayo siku hizi yanahifadhiwa katika ahadi na nyingi huwa batili,” aeleza.

Baadhi ya watu hukosa kutofautisha ahadi za kweli na za uongo na kujikuta wamezama katika uchumba usiojengwa katika msingi imara.

Bi Moraa asema wapenzi hutumia maneno teule kuelezea hisia zao wanapowaahidi wachumba wao yasiyotekelezeka.“Kubadilishana ahadi ni hatua inayokoleza penzi utamu. Hata hivyo, athari zake zaweza kuwa mbaya ahadi zisipotimzwa,” asema. Kulingana na mtaalamu huyu ni muhimu mtu kumwahidi mchumba wake anayoweza kutimiza.

“Wakati wa ushauri, tunawaeleza wanandoa utaratibu uliopo na mambo haya ya kuwekeana ahadi ambayo yamekuwa mwiba katika ndoa nyingi yasipotimizwa,” asema.

Anaeleza kwamba watu wengi hukosea kwa kutaka watimiziwe ahadi walizopatiwa na wachumba wao katika muda mfupi au kwa vitisho na kuwawekea presha.

“Ndoa ni ya muda mrefu na baadhi ya ahadi huchukua muda kuafikiwa japo watu wengi hawaamini haya na kuwasikia wenzao na haya kuwatisha,” asema.

Wataalamu wanasema watu wengi wanaamini ahadi ni nguzo ya mapenzi na thibitisho kamili la huba na kutozitimiza ni kuonyesha kwamba moto wa mapenzi huwa umezima.

Mshauri wa maswala ya nikahi Bi Joyce Mumbi wa shirika la Big Hearts jijini Nairobi anasema zikitimizwa bila presha ahadi huzuia mitafaruku katika ndoa.

“Hizi ni zinazowekwa bila shinikizo, kwa nia njema na zinazoweza kutimilika, “ aeleza. Mwandishi maarufu wa tungo za mahaba Meleanie Henson anasema kwenye tovuti ya oneheartwedding kwamba ubadilishanaji wa ahadi unajenga msingi thabiti wa ndoa.

Ni kauli ambayo Linda Bardes, anayejulikana mtandaoni kama The wedding coach anakubaliana nayo kwenye makala yaliyochapishwa katika tovuti ya weddingvowsandceremonies.com. Linda anasema kwamba ahadi za uchumba hudumisha moto wa mahaba.

Anasema kutoa ahadi kunahitaji mhusika kujielewa kwanza, ndoto zake na za mchumba wake na anayotaka kutimiza katika maisha ya ndoa.

“Unapotoa ahadi, elezea ndoto zako, malengo uliyonayo, mahaba, pesa, familia na hata nyumba ukizingatia mwenzako,” asema. Katika kauli za wataalamu wengi wanakubaliana kuwa zikitumiwa vyema na kutolewa katika mazingira yanayofaa ahadi za uchumba zinachangia katika kukuza uhusiano wa kimapenzi.