Ahepa mkewe kuhusu bajeti kali ya Krismasi

Na TOBBIE WEKESA

Imepakiwa - Sunday, December 17  2017 at  13:51

Kwa Muhtasari

CHAKOLI, TESO

KIZAAZAA kilizuka eneo hili, baada ya kipusa kumpa polo bajeti ya krismasi. Kulingana na mdokezi, polo alimzomea kipusa huku akimkumbusha jinsi maisha yalivyomkalia vibaya mwaka mzima.

 

Kipusa hakufurahishwa na matamshi ya polo. “Maisha gani yamekuwa magumu! Mwaka ulipoanza ulikuwa mlevi. Kwa mama pima hujakuwa ukikosa. Ukora utaacha,” kipusa alimkaripia polo.

Duru zinasema kipusa alimlazimisha polo kuipokea bajeti hiyo. “Chukua haraka. Hivi vitu navihitaji kesho kutwa. Nusu yake navipeleka kwetu hata mama yangu pia afurahie kidogo,” kipusa alimueleza polo.

Penyenye zinasema polo alipoona kipusa amezidi, aliamua kutafuta mbinu ya kuhepa jukumu hilo.
Polo alibeba suruali zake tatu na shati kadhaa na kuanza safari. “Nitarudi jioni. Hivi vitu vyote umeniambia nilete nitaleta. Usijali,” polo alimueleza kipusa huku akianza safari.

Kipusa alishangazwa na polo na kumuuliza alikokuwa akienda.

Polo aliendelea na safari yake bila kujali maneno ya kipusa. “Hii begi naenda kubebea vitu vya krismasi. Nitarudi jioni. Jipange kuenda kwenu kesho kutwa,” polo alimueleza kipusa.

Bila kujua kilichokuwa ndani ya begi, kipusa aliamua kumwamini polo. Jioni ilipofika, polo hakuonekana. Kipusa alipompigia simu, polo hakuchukua ila alituma ujumbe.

“Hebu jipange hii krismasi. Mimi siko karibu. Tutaonana mwaka ujao Desemba,” ujumbe ulisema.

Kipusa naye alimshtumu polo kwa uamuzi wake. “Una ujinga sana. Hivyo vitu vichache tu ndivyo vinakufanya utoroke boma. Umejiaibisha mwenyewe,” kipusa alimzomea polo.

Polo alimgombeza kipusa kwa kuwajali watu wa kwao tu. “Siwezi kuwalisha watu wa kwenu. Hebu jipange. Tutaonana mwaka ujao,” polo alimueleza kipusa huku akiizima simu yake.