Aibu ya mwaka kwa mwalimu kudaiwa madeni na wanakijiji hadharani

Na DUNCAN MWERE

Imepakiwa - Saturday, May 14  2016 at  13:09

Kwa Muhtasari

MUKARO, NYERI

Shughuli katika shule moja ya msingi zilisimama kwa muda wa saa mbili baada ya mwalimu mmoja kudaiwa madeni na wanakijiji wa eneo hili.

 

SHUGHULI katika shule moja ya msingi zilisimama kwa muda wa saa mbili baada ya mwalimu mmoja kudaiwa madeni na wanakijiji wa eneo hili.

Mwalimu huyu aliyehudumu katika shule hiyo kwa zaidi ya miaka ishirini inaaminika hutangamana na wenyeji wa hapa kiasi cha kwamba huwatembelea nyumbani mwao baada ya masomo na wakati hana vipindi.

Wanakijiji waliokuwa na hasira walimininika shuleni mwendo wa asubuhi huku wakidai haki yao. Kioja hiki kilivutia walimu, wanafunzi na wanakijiji wa kata hiyo na kukatiza shughuli za masomo kote shuleni.

“Haki yetu! Lazima alipe bidhaa zetu ambazo tumemkopesha kwa muda wa nusu mwaka,” wanakijiji waliokuwa na ghadhabu wakapaza sauti. Wengine walisema hawatabanduka shuleni hadi wapatiwe haki yao.

Haya yakijiri mwalimu mkuu alikuwa ofisini akiwa mwingi wa matumaini shida hii itatatuliwa na naibu wake na mwalimu wa zamu. Maji yalipozidi unga ilibidi mwalimu mkuu kuingilia kati ili kupata suluhisho.

Hapo ndipo mambo yalichukua mkondo mpya na joto lililokuwa limepanda kupunguza. “kwanza lazima mtulie kwani sheria za taasisi hii haziruhusu wananchi kuzua rabsha hapa shuleni wakati wowote,” akaonya mwalimu mkuu.

Wote waliokuwa wakipayuka walifyata ulimi kwani walielewa ima fa ima wao ni wazazi shuleni humo. Mkuu wa shule hii aliwaita walimu na baadhi ya wazazi waliokuwa wakidai haki zao.

Wakati wa kikao hicho ambacho nusra kitimbuke kutokana na malumbano kutoka pande zote mbili. Kwa tajriba na hekima ya mwalimu aliweza kukomesha ugomvi huu uliokuwa umezidi.

“Mbona msifuate kanuni na utaratibu unaofaa kutatua tofauti kati yenu,” akauliza mwalimu mkuu akionyesha kukerwa na tukio hilo ambalo halijawahi kutokea shuleni humo tangu ajiunge nayo. Wanakijiji hao walisema wamekuwa wakiahidiwa ahadi za kulipwa na wakaona wanachezewa shere.

"Tumesubiri kwa muda wa siku, miezi na miaka lakini kila wakati tunaambulia patupu,” akasema mmoja wao aliyekuwa mkuu wao. “Kwani

mnadai nini na nini, " akahoji mwalimu mkuu aliyekuwa katika nafasi ya hakimu.

Kila mmoja aliyepata fursa alisema si mara moja aliwahi kumkopesha bidhaa na aina mbalimbali ya vyakula na kukosa kulipwa. Wengine walieleza kuwa waliwahi kumkopesha viumbe ambao hufugwa ila hakuna malipo wamewahi kupata.

Kuku na mbuzi

“Mimi niliwahi kumkopesha kuku wawili na mbuzi lakini kufikia sasa ni muda wa miezi minane na sijapata haki yangu,” akasema mama mmoja. Madai yaliendelea huku mazungmzo yakionekana kutokamilika kwa muda uliotengewa. Taharuki ilizidi kutandaa shuleni kila mmoja aliyekuweko akionekana kujua hatima ya kesi hiyo.

Hatimaye, mwalimu mkuu aliwaomba wanakijiji hao kuandika ni nini wanamdai mwalimu huyo. Baadaye walikubaliana ni lini na ni wapi watapata haki yao na wakaonywa na mwalimu mkuu kuwa macho wanapokopesha walimu na mtu wa aina yoyote bidhaa zake. Kwa mujibu wa wale wanaomfahamu mwalimu walisema halipi madai hadi sheria itumike.

Wanakijiji waliondoka wakiwa na wingi wa matumaini kupata haki yao. Baadaye mwalimu mkuu aliandaa kikao na walimu wote na kuwashauri kuhusu baadhi ya mambo ambayo yatawashushia heshima yao.

Hatimaye alimwita mwalimu mhusika na kumwonya endapo hatabadilisha mienendo yake huenda atapata uhamisho.