Machozi yamtoka ajuza kuona ndevu za pasta zinafanana na beberu wake aliyeibwa

Imepakiwa Tuesday May 3 2016 | Na DUNCAN MWERE        

Kwa Muhtasari:

MUTHINGA, Nyeri

Ajuza mmoja katika sehemu hii aliwashangaza waumini na mhubiri kwa kuwa na huzuni wakati wa ibada. Mwanamke huyo alifika kanisani mapema ilivyo desturi yake lakini hakuwa mchangamfu.

AJUZA mmoja katika sehemu hii aliwashangaza waumini na mhubiri kwa kuwa na huzuni wakati wa ibada. Mwanamke huyo alifika kanisani mapema ilivyo desturi yake lakini hakuwa mchangamfu.

Waumini wenzake hawakujua mwenzao ambaye hakosi kuhudhuria ibada na mikutano ya injili katikati ya juma alikuwa na jambo ambalo limemwendea mvange.

Wakati wa nyimbo za sifa mama huyu mwenye watoto wanane aliimba ilivyo desturi yake. Ilipowadia wakati wa ushuhuda mama huyu hakujitokeza kushuhudia  kwani kila fursa inapopatikana huwa mstari wa kwanza na  anafahamika kuwa kielelezo bora cha kuigwa na vijana wa kanisa hilo.

Kipindi cha mahubiri kilipofika, mhubiri aliyealikwa kutoka parokia jirani alisimama na kujitambulisha. Alikuwa mrefu na mwingi wa maneno ya hekima yaliojikita kwenye biblia takatifu.

Fauka ya hayo alikuwa amefuga msitu wa ndevu ambazo zilitoa taswira ya mitume wanaosimuliwa kwenye misahafu.

Alianza mahubiri yake yaliokuwa na ucheshi na taharuki huku waumini wakionyesha ishara ya kutaka  aendelee. Akiwa katikati ya ibada aligundua kuna mama mmoja aliyekuwa na huzuni.

Ajuza huyu alishika tama kwenye shavu lake la kushoto na kububujikwa na machozi. Ni mhubiri huyu pekee aligundua kuna jambo ambalo linaenda kombo ila alijitia hamnazo na akaendelea na mahubiri yake.

Kadri mahubiri yalivyoendelea ndivyo huzuni ilimzidia ajuza huyu. Kufumbua na kufumbua akashika tama katika shavu lake la kulia na kudodokwa na machozi. Hatimaye ibada ilifika ukingoni nao waumini walifumukana.

Katika pilkapilka za kuondoka mhubiri aliamua kumuuliza ajuza tatizo alilokuwa nalo kutoka awali hadi akheri. “Mbona ulikuwa na huzuni wakati mahubiri yalikuwa yakiendelea,” akauliza mhubiri aliyekuwa na hamu ya kutaka kujua.

“Nilipokuona ukihubiri nilikumbuka beberu wangu aliyeibiwa na wezi  na alikuwa na ndevu sawa na zako,” akajibu mama aliyekuwa mwingi wa huzuni na masikitiko. Kisha mhubiri alimpatia pole na kumuomba awasamehe wezi waliomwibia beberu wake.    

Share Bookmark Print

Rating