Akasirikia pasta kwa kukataa kumfanya mpishi wake

Imepakiwa Wednesday November 15 2017 | Na  JOHN MUSYOKI

Kwa Muhtasari:

Ngetani, Masinga

KIOJA kilishuhudiwa sehemu hii mama mmoja aliponunia pasta wake kwa kutomchagua kuwa mpishi jikoni kila Jumapili.

Inasemekana mama alikuwa jirani wa karibu wa pasta lakini alikasirika pasta alipokataa kumchagua kuwa mpishi. Mama alishindwa kuzuia hisia za machungu na kusikika akifoka baada ya kuchujwa na pasta.

“Yaani pasta amenipuuza tu na mimi ni jirani yake, hataki niwe mpishi. Wallahi ameniudhi sana na kuanzia leo sitaongea naye wala kumpa salamu zangu. Ajipange na kwangu asiwahi kutia guu kwa sababu nitahama niende kanisa nyingine,” mama alisema.

Inasemekana waliomsikia akipayuka walipigwa na mshangao mkubwa na kumshauri huku wengine wakitia chuki na kuangua vicheko.

“Pole sana dada yangu. Badala ya kununa heri uende ukapikie familia yako. Kwani ukipikia pasta utapata faida gani. Sio lazima uwe mpishi wa pasta hata kama wewe ni jirani wake wa karibu,” muumini mmoja alimwambia mama huku wengine wakiangua vicheko.

Inasemekana ibada ilipoisha mama alitangulia kuondoka kanisani na haijulikani iwapo alirejea katika kanisa hilo tena.

Share Bookmark Print

Rating