Ashindwa ampe mke yupi zawadi aliyopewa na rafikiye

Imepakiwa Wednesday May 17 2017 | Na DENNIS SINYO

Kwa Muhtasari:

Mosoriot, NANDI

MZEE mwenye wake wawili alitokwa na kijasho aliposhindwa ni mke yupi wa kumpa zawadi aliyotunukiwa na rafiki yake.

Jamaa huyo alikuwa ameandamana na wake wawili kwenye sherehe aliyoalikwa na rafiki yake wa dhati.

Kulingana na mdokezi, wake hao walikuwa wakigombana mara kwa mara wakiwa nyumbani. Walipowasili kwenye sherehe hiyo, waliketi karibu na mumewe licha ya uhasama wao wa muda mrefu.

Kabla ya kutamatisha sherehe, mwenyeji wao alianza kuwatuza wageni wake aliodai walikuwa wamesimama naye kwa miaka mingi.

“Jamaa aliitwa kupatiwa blanketi kama zawadi. Mke wake wa kwanza alimfuata kwenye jukwaa naye mke wa pili akaingiwa na wivu na kumfuata pia. Alipopewa zawadi yake, jamaa huyo alishindwa ni mke yupi wa kumpa kwani wote wawili walikuwa wamesimama na yeye pamoja,” alisema mdokezi.

Inaarifiwa wanawake hao walikuwa wamenyoosha mikono kupokea zawadi hiyo ila jamaa akahisi kwamba angesababisha balaa kama angempa mmoja na kumwacha mwingine.

Wageni waliokuwa wameketi walitazama kioja hicho kwa muda kabla ya mwanaume huyo kuamua kushikilia zawadi hiyo mwenyewe mkononi hadi alipotoka kwenye jukwaa.

Share Bookmark Print

Rating