Atandikwa na sponsa kwa kunyemelea asali

Imepakiwa Monday May 29 2017 | Na SAMMY MURAYA

Kwa Muhtasari:

MABROS, GITHURAI

SINEMA ya bure ilishuhudiwa katika duka moja mtaani hapa kalameni alipoangushiwa mangumi mazito na buda kwa kumpata akitongoza mpango wake wa kando katika biashara aliyomwekea.

Yasemekana polo alizoea kumtembelea kimwana huyo katika biashara yake kumrushia mistari ya mapenzi. “Jamaa alikuwa ameonywa na kidosho huyo kwamba alifadhiliwa kuanzisha biashara na sponsa wake, lakini hakusikia la mwadhini wala la mteka maji msikitini,” alisema mdokezi wetu.

Duru ziliarifu meza ya dondoo kwamba siku ya kioja, polo alienda katika duka la mwanadada huyo kumrushia mistari ya mapenzi kama ilivyokuwa kawaida yake. Inasemekana siku hiyo kipusa hakutaka kuongea na jamaa. “Hae, nimekuja, ni muda sijakuona.” kalameni alimueleza mwanadada.

Kulingana na mdokezi, kidosho alikimya na kujaribu kumuepuka jamaa. Muda wa kuku kumeza punje ya mahindi, gari la kifahari lilifika na kuegeshwa karibu na duka hilo na buda aliyeunga akashuka.

“Wewe ndiye nasikia huwa unasumbua mke wangu?” mzee huyo aliuliza. “Ati mke wako? Miaka yako na ya mrembo huyu haiambatani,” kalameni alimjibu kwa dharau.

Kabla ya jamaa kuongeza neno, mangumi na mateke yalimshukia akaramba sakafu. “Ukijitazama kuanzia utosini hadi unyayoni unaweza kutunza mwanamke kama huyo?” aliuliza buda akihema kwa hasira.

“Huwa namkanya aache kuja hapa na humweleza mimi ni mke wa mtu lakini huwa hasikii,” alishtaki kipusa huyo.

Kalameni huyo ambaye alizidiwa na kichapo hakuwa na budi ila kuchukua gari nambari mguu niponye na kutimka kama swara huku waliotazama kioja hicho wakicheka.

Share Bookmark Print

Rating