DONDOO: Kimada na mama boi wapapurana hadharani

Na TOBBIE WEKESA

Imepakiwa - Thursday, March 2  2017 at  15:08

Kwa Muhtasari

OL KALOU, Laikipia

KIZAAZAA kilizuka eneo hili baada ya kidosho kumvamia mke wa polo akimlaumu kwa kumzuia mumewe kumuoa mke wa pili.

 

Kulingana na mdokezi, kidosho alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na polo. Inasemekana polo alikuwa amemuahidi kidosho kuwa atamuoa awe mke wake wa pili.

Duru zinasema kidosho alipoona kuwa polo alikawia sana kutekeleza ahadi yake ya kumuoa, aliamua kumkumbusha. “Nakumbuka ulikuwa umeniahidi kuwa mwezi huu tutaishi pamoja. Ninapokuona ni kama huna dalili zozote,” kidosho alisema.

Inasemekana kuwa polo alimueleza jinsi alivyozomewa na mke wake nyumbani. “Mimi hata sijui ni nani alimuambia mama boi eti napanga kukuoa. Amenizomea sana,” polo alimueleza kidosho.

Kulingana na mdokezi, polo alimueleza kidosho awe na subira hadi mkewe atakapotulia. “Kwani huyo mwanamke ndiye hukuamlia cha kufanya?” kidosho alimuuliza polo kwa hasira.

Inasemekana kidosho alielekea hadi kwa boma la polo na kuanza kumshambulia mkewe kwa maneno. “Wewe una shida gani? Kama humlindi bwana wako vizuri acha kumpa masharti,” kidosho alimuonya mke wa jamaa.

Duru zinasema mama alimuonya kidosho aachane na mumewe kabisa. “Acha ujinga. Nani alikuambia simlindi vizuri bwanangu? Porojo sitaki. Kwenda huko. Sikutaki katika hili boma,” alimzomea kidosho.

Kulingana na mdokezi, wawili hao walianza kurushiana matusi huku majirani wakibaki kutazama sinema ya bure. “Upende usipende lazima nitaolewa katika hili boma. Huna uwezo wa kumzuia mumeo kuoa,” kidosho alifoka.

Habari zilizotufikia zinasema karibu wawili hao wakabane koo. “Sitaki usaidizi wowote kutoka kwako,” mama alimuonya kidosho.