http://www.swahilihub.com/image/view/-/2882660/medRes/360614/-/1009n12/-/KTflowers.jpg

 

FUNGUKA: Sina muda na wanaume wangwana

Wapenzi

Wapenzi wakiwa wameshika maua. Picha/MAKTABA 

Na PAULINE ONGAJI

Imepakiwa - Wednesday, November 8  2017 at  11:21

Kwa Muhtasari

MABINTI wengi na hasa wa kisasa watakubaliana nami kuwa hakuna kitu ambacho mwanamke hufurahia kama kubembelezwa na kudekezwa katika uhusiano.

 

Wanawake wengi watakuambia kuwa wanataka mwanamume anayewafungulia mlango, kuwavutia kiti, kuwaletea chokoleti na maua wakati wa maadhimisho ya siku za kuzaliwa na Valentino, na kupelekwa miadi mara kwa mara.

Mwanamume ambaye yuko tayari kukumbatia na kukubembeleza kila unapoonyesha ishara za kutiririkwa na machozi. Lakini kwa Melisa, binti wa umri wa miaka 30, mambo ni tofauti sana. Kwanza kabisa binti huyu ni msomi kwani ana shahada ya uzamili kutoka mojawapo ya vyuo vikuu vinavyotambulika nchini.

Kadhalika ana ajira nzuri na ukimwona jinsi alivyo kutoka kwa mavazi, mitindo ya nywele na hata gari analoendesha ambapo anaonyesha sura kamili ya binti wa kisasa.

Lakini kipusa huyu kamwe hafurahii “kubembelezwa” huko kwa wanawake huku akiwaita wanaume wanaofanya hivyo kuwa dhaifu. Hana haja ya kupelekwa miadi, kununuliwa maua na chokoleti mara kwa mara au hata kudekezwa.

Yeye anafurahia penzi hatari, uhusiano unaohusisha vita vya mara kwa mara, suala ambalo anasema linathibitisha uhusiano wa kimapenzi au ndoa.

“Nataka mwanamume mwenye nguvu, kaka anayenizaba makofi mara kwa mara kunikumbusha kila ninapokosea, ishara ya kwamba hatari ikitokea yuko tayari kunilinda.

Mwanamume akiwa mnyenyekevu na kumbembeleza mwanamke kila mara hauna hakikisho kuwa endapo mtu atakushambulia atakuwa na nguvu ya kukulinda.

Sitaki mwanamume anayejipuuzilia marashi, kaka anayejipaka mafuta au dume lililo na mikono miororo hata kuliko mabinti.

Mwanamume anapaswa kuwa na kifua kipana na hata awe anavunda jasho, awe anafanya kazi afisini au ya mikono. Nataka wanaume wenye nguvu, kaka anayenichapa mara kwa mara kunihakikishia kuwa yeye ni kichwa cha nyumba.

Mwanamume asiyeomba msamaha wala kugusa kazi za nyumbani, dume lisiloingia jikoni na badala yake linakaa sebuleni likisubiri kuletewa chakula na mkewe.

Pindi akiingia nyumbani anaamrisha kuvuliwa koti, viatu na hata soksi. Mwanamume asiyeomba na kunyenyekea. Dume linalokurushia matusi huku na kule na kukumbusha iwapo umekosea.

Mwanamue ambaye kila jioni anataka chakula kilichopikwa nyumbani badala ya kuharibu pesa akikupeleka mkahawani eti kwa miadi.

Kwangu wanaume wanaofanya mambo kama vile kuwapeleka wake au wapenzi zao miadi, kuwanunulia maua na kuwabembeleza huku na kule ni dhaifu na hawastahili wanawake kamili.

Hao ni madume wanaostahili wasichana wadogo wa vyuoni kwani wao ni dhaifu. Sitaki maua kwani mie sio nyuki, na wala sitaki chokoleti kwani hiyo inaonyesha kuwa dume hilo halina ustadi wa kuangusha mistari pasipo kutumia vitu vitamu.”