Fundi alishwa makonde kwa kuvalia viatu vya kastoma

Imepakiwa Wednesday March 30 2016 | Na TOBBIE WEKESA

Kwa Muhtasari:

DANDORA, Nairobi

FUNDI mmoja wa viatu mtaani hapa, alijipata pabaya baada ya kupatikana akivaa viatu vya kastoma.

Inasemekana kuwa fundi alikuwa akitoka sokoni na akaamua kupitia kwa mama pima alikomkuta polo mwenye viatu akijiburudisha kwa kileo.


“Fundi leo unakaa smati sana. Hiki kiatu kiko chonjo tu sana. Ulikinunua wapi?” polo alimuuliza fundi.


Inasemekana kuwa fundi hakujibu swali hilo. “Badala yake alijaribu kuleta hadithi nyingine ili kukwepa kumjibu polo. Lakini polo aliendelea kumuuliza maswali hadi alipopewa jibu sahihi,” alieleza mdokezi.


“Unasema kiatu hiki ni cha kastoma wako ambaye alikawia kuleta pesa. Na hata mimi nilileta viatu vyangu vinavyofanana na hivi kwako ushone. Sijui kama umemaliza kushona?” polo alimuuliza fundi.


“Mimi huwa sijali. Mtu akileta kiatu kushonewa na akawie kuleta hela, nazitumia tu,” fundi alieleza.


Inasemekana kuwa polo alizidi kuuliza maswali na kuhakikisha kuwa fundi alikuwa amevalia viatu vyake, mzozo ulianza.


“Wewe kichwa chako hakifanyi kazi. Nimekuletea viatu jana kisha baada ya kushona umevivaa,” polo alimzomea fundi.


Kulingana na mdokezi wetu, polo alitaka kumtoa fundi viatu miguuni. “Ebu toa hivyo viatu miguuni mwako haraka. Kama ni pesa zako nakupa saa hizi,” polo alimueleza fundi.


“Njoo nyumbani kwangu utavipata huko. Siwezi kutembea bila viatu hadi kwangu.” fundi alimueleza polo.


Inasemekana kuwa polo hakukubaliana na fundi. “Aliinuka tayari kumzaba makofi lakini watu waliokuwa karibu naye wakamkamata,” alieleza mdokezi.


“Na wewe pia, umezoea tabia mbaya. Viatu vya wateja wako si vyako. Itabidi uwaheshimu,” mzee mmoja alimweleza.
Ilimbidi fundi apotee kabla ya mambo kuharibika zaidi.

Share Bookmark Print

Rating