Jombi ajuta kuwatuma watoto karo kwa wakwe zake

Na DUNCAN MWERE

Imepakiwa - Monday, May 9  2016 at  17:59

Kwa Muhtasari

KIAMAINA, NYERI

Jombi mmoja kutoka eneo hili aliyekuwa na mazoea ya kuwatuma wanawe kwa wakwe zake kuchukua

karo na mahitaji mengine alijipata pabaya baada ya kuzomewa na wanakijiji.

 

Jombi mmoja kutoka eneo hili aliyekuwa na mazoea ya kuwatuma wanawe kwa wakwe zake kuchukua karo na mahitaji mengine alijipata pabaya baada ya kuzomewa na wanakijiji.

Mwanamume huyu mzembe kutoka eneo hili aliwaeleza watoto wake endapo wametumwa nyumbani kwa sababu ya pesa za matumizi shuleni wawe wanaendea kwa wakwe wao.

Ujanja wake uligunduliwa na wanakijiji walipoona watoto wa mzee huyu wa umri wa makamo wakifika boma la wakwe wake wakati vipindi vya masomo vinaendelea.

Awali walidhani kuwa ni mapenzi watoto walikuwa nayo kwa upande ambao mama yao ametoka. Lo! Majibu waliyopata yaliwaacha vinywa wazi kwani watoto hao walio na umri wa miaka kati ya miaka tisa na kumi na mmoja walisema wanaelekezwa na baba yao.

“Baba yangu hutushauri kuendea karo na matumizi mengine katika boma ambalo mama ametoka,” akasema mmoja

wa watoto hao aliye na umri mkuu kati yao.

Kina mama walioona fedheha na kuwaliamuru watoto kwenda makwao na kumhimiza babake kuwajibika. Wakati wa adhuhuri watoto walifika nyumbani na kumkuta baba yao.

Alipowaona wanaye alishangaa sawa na mtu aliyeona sinema ya shani. Baada ya kuwahoji wanaye alimaizi kuwa kitumbua kimeingia mchanga.

Kwani mambo yameendaje mkaja nyumbani ilhali siku zote nimewaelekeza boma ambalo mama yenu ametoka?" akauliza jombi huyo. Watoto waliojawa na woga hawakumfamisha babake ujanja wake umegunduliwa na wanakijiji wenzake.

Aliwarai watoto kwenda kwa wakwe wake kwa azma ya kupata karo. Watoto walishika kiguu na njia na kwenda kule walizoea.

Raundi hii watoto walionekana na wanakijiji wengi kuliko ilivyokuwa hapo awali. Waliamua ni lazima mzee huyu ajue kilicho na mwanzo kina mwisho wake.

Waliamuru watoto kurudi makwao ili mahitaji yao yatimizwe na mzazi wao. Kwa nyota ya jaha walimpata baba watoto akibarizi nje ya boma yake.

Alijaribu kujitetea lakini yote yalikuwa bure bilashi kwani walimweleza kinagaubaga kuwajibikia watoto wake kwa vyovyote vile.