Jombi alisha watoto mijeledi kwa kufikiri walimwita 'punda'

Na DUNCAN MWERE

Imepakiwa - Monday, May 9  2016 at  18:10

Kwa Muhtasari

GITERO, NANYUKI

Watoto wa familia moja katika kitongoji hiki wanajuta baada ya kuadhibiwa vikali na baba yao kwa kutumia lugha ambayo haelewi.

 

Watoto wa familia moja katika kitongoji hiki wanajuta baada ya kuadhibiwa vikali na baba yao kwa kutumia lugha ambayo haelewi.

Kisa hiki kilijiri wakati watoto waliendelea kutumia lugha hiyo ambayo baba hakuelewa katu. Lililomuudhi baba yao ni kuwa wanawe walitumia maneno ya kumshushia hadhi na kumpiga majembe jambo ambalo lilimfanya kupandwa na mori na kuchukua hatua kali. Baba yao ambaye

alidhani baadhi ya maneno hayo ni ya kumtusi.

Aliwaonya vikali watoto hao ambao wanaelewa maneno ya lugha kadri yanavyochipuka kila uchao. Mdokezi wetu alidokeza mwandishi wa Swahilihub kuwa vijana hao wameathirika si haba na hiyo lugha ya mjini almaarufu Sheng.

“Popote wawapo vijana hawa wana mazoea ya kutumia lugha hii jambo ambalo limechangia kukosana na watu kijijini ambao katu

hawaelewi lugha hii,” akasema.

Penyenye ziliarifu kuwa ni kutokana na mazoea haya wameathirika shuleni. “Imekuwa ni kawaida ya walimu wao kulalamika kila wakati kutokana na wanafunzi hao kutumia lugha batili hususan katika uandishi wa insha,” akaeleza mmoja wa walimu kutoka katika eneo hilo wanakosomea watoto hao.

Kilichomkera babake ni namna walivyozoea kumwita. Mmoja wa vijana hao alifika nyumbani na kuuliza babake endapo kulikuwa na chochote cha kula. “Wewe buda leo kuna msosi nimange ,”? kijana akauliza.

Matusi

Swali hilo lilimkasirisha baba mtu na kuamua kumpatia adhabu ambayo hataisahau maishani mwake. “Mbona unanitusi punda ilhali mimi ndiye babako mzazi?,” akauliza babaye.

Kijana alijaribu kujitetea lakini yote yaliaambulia patupu. “ Mimi nimesema buda lakini sijasema punda,” akajitetea. Mara ghafla babake aliwaita watoto wengine ambao waliitikia kwa lugha hiyo bila kumaizi wamerusha jiwe kwenye kituo cha polisi.

“Niaje mbuyu kwani kulikoni,” wakaitikia. Kwa hasira za mkizi baba ambaye hakuonyesha utani wala mzaha aliamua liwe liwalo lazima awatie adadu na wajue kilichomtoa kanga manyoya.

“Leo ni leo msema kesho ni mwongo, lazima mjue kwa nini sangara akachomwa moto," akaeleza bila dhihaka. Baba alichukua bakora na kuwatandika watoto na kuwaonya wasiwahi kutumia lugha Sheng karibu naye na mazingira ya nyumbani mwake.