Jombi atandikwa kofi na mke kwa kumwaga mtama

Imepakiwa Wednesday May 24 2017 | Na TOBBIE WEKESA

Kwa Muhtasari:

Masinga, MACHAKOS

KIOJA kilizuka eneo hili baada ya polo kuzabwa kofi kali na mkewe akimlaumu kwa kuwafichulia ndugu zake tabia zake.

Kulingana na mdokezi, ndoa ya wawili hawa ilikuwa na msukosuko mwingi sana kwani kila wakati walikuwa wakigombana.

Inadaiwa ugomvi wao ulitokana na madai kwamba kipusa alikuwa na macho ya nje. Duru zinasema polo alikuwa akipata habari kutoka kwa majirani jinsi wanaume walipokuwa wakiingia kwake akiwa kazini.

Inasemekana polo alijaribu kumuuliza kipusa iwapo madai ya majirani yalikuwa ya kweli. “Achana na hizo porojo za watu. Lakini kumbuka pia mwanamke anahitaji kutunzwa,” kipusa alimueleza polo.

Duru zinasema jibu la mwanadada lilimchoma polo rohoni. “Sasa unasema mimi sikutunzi vizuri?” polo alimuuliza kipusa. 

Inasemekana polo aliwaita ndugu za kipusa. “Nimewaita kwenye kikao hiki ili niwaeleze tabia ya dada yenu,” aliwaeleza mashemeji zake.

Kulingana na mdokezi, polo aliwaeleza mashemeji zake yote kumhusu dada yao mbele ya mkewe mwenyewe.

Penyenye zinasema baada ya polo kutoa kauli zake, mkewe alisimama na kuelekea alikokuwa polo. 

“Huyu mtu anadai eti mimi nina mipango ya kando, umewahi nipata na mmoja? Mbona unaniaibisha hivyo? mama alimkaripia polo.

Duru zinasema kabla ya polo kujibu swali, kipusa alimzaba kofi moja kali sana lililomuacha akibabaika. “Wuuui. Ameniumiza,” polo alilia.

Inasemekana kipusa alikula kona huku akiwaacha ndugu zake wakimpa polo huduma ya kwanza. 

“Na akipona mwambieni ujinga ndio mimi sipendi. Yeye hata kunitunza hawezi. Halafu ananiaibisha hadharani eti mimi namcheza. Hata yeye acha apate aibu kidogo,” kipusa alisema huku akienda zake.

Share Bookmark Print

Rating