Kalameni afurushwa chamani kwa dai ni mpishi

Na DUNCAN MWERE

Imepakiwa - Monday, May 9  2016 at  18:25

Kwa Muhtasari

BUSARA, NYAHURURU

Mwanamume mmoja kutoka mji huu alitimuliwa kwenye kikao cha wazee kwa madai hupenda kuingia jikoni kwa lengo la upishi.

 

Mwanamume mmoja kutoka mji huu alitimuliwa kwenye kikao cha wazee kwa madai hupenda kuingia jikoni kwa lengo la upishi.

Jombi huyu ambaye ni baba wa watoto wanne inasemekana hupenda kuingia jikoni kujipikia ilhali mkewe huwa tayari kutekeleza wajibu na majukumu yake barabara.

Uvumi ulianza wakati watoto wake walipoanza kutangazia wenzao mienendo ya babaye. Fununu hizo zilienea si shuleni si nyumbani almuradi watu wa matabaka mbalimbali walikuwa na mwao kuhusu jombi huyu ambaye inasadikika hupenda mlo kupindukia.

Kwa mujibu wa watoto, waliwambia wengine wakati walikuwa wakirudi nyumbani. Hatimaye ujumbe huu uliwafikia wazazi kisha habari zikaenea mithili moto kwenye kichaka kikavu.

“Unajua baba ameteka majukumu ya mama haswa upishi kila wakati," akasema mmoja wa watoto hao.

Watoto wenzake walisaili zaidi ili wapashwe kuhusu baba yao. Udaku huu uliwafikia wazee wa rika lake na kuamua kuwa na kikao na mpishi huyo hodari. Baada ya kuhojiwa na wenzake aliungama bila kusita na kuamuliwa kukaa kando ili uamuzi wa busara utolewe.

Kisha aliitwa ili kujua hatima yake. Mkuu wa kikao hicho alimweleza namna baraza liliamua. Kabla ya hukumu kutolewa jombi huyu aliulizwa endapo yuko tayari kukomesha mienendo yake.

Uraibu wa kupika

“Mimi siko tayari kuacha kupika kwani huu ni uraibu wangu,” akajibu. Mzee huyu alisema yuko tayari kwa lolote lakini ataendelee na hulka yake anayopenda na kuienzi mithili ya moyo yake.

Mkuu wa kikao hicho aliye pia mzee wa kijiji alisimama na kutoa wosia kuhusu majukumu ya mwanamume kuhusu jamii hiyo.

“Kwanza ni lazima mjue kuwa tangu jadi mwanamume hakuruhusiwa kuingia jikoni, endapo kulikuwa na jambo la dharura rafikiye mkewe akiaalikwa ili kuwajibika,” akashauri.

Ni kweli kuwa mwenzetu anatutia doa kutokana na tabia ambazo zinatukera sisi sote,” akaongezea. Wakati wa kutolewa hukumu wazee wenzake walioonekana kuunga mkono uamuzi uliotolewa dhidi ya kalameni na fauka ya hayo hakuonyesha wasiwasi wowote.

"Kwa vile afua ni mbili, lazima uchague moja kati ya hizi kulipa kondoo watano au kupigwa marufuku chamani wala kushiriki mikutano wa kijiji hicho,” akaongezea.

Mzee mpishi alisimama na kusema. “ Mimi nimeamua kutolipa ada yoyote lakini nitakuwa nikihudhuria mikutano ya wazee kwenye baraza,” akajibu.

Jawabu hilo liliwafanya wazee hao kupandwa na mori na kumchukulia hatua kali. “Kutoka leo hutakuwa ukishiriki mikutano ya wazee wa kitongoji hiki na huo ndio uamuzi wa jopo na wazee wenzangu,” akaongezea.

Kutoka siku hiyo hiyo mzee mpishi hajakuwa akihudhuria mikutano wala kushirikishwa katika maamuzi ya baraza la wazee.