Kalameni ahama ploti mke kuolewa na jirani

Na  EDISON WANGA

Imepakiwa - Wednesday, November 1  2017 at  06:23

Kwa Muhtasari

CHAANI, MAGONGO

JAMAA wa hapa aliamua kuhama ploti baada ya kugundua mkewe waliyetengana naye alikuwa ameolewa na jirani yake.

 

Duru zilizotufikia zinasema kuwa jamaa ambaye ni mlevi, alishindwa kukidhi mahitaji ya familia na akawa anarudi nyumbani usiku wa manane kumpiga mkewe akitaka chakula.

Ilibidi mkewe afanye vibarua ili kupata riziki. Jamaa hakujali hayo. Aliendelea kumpiga mkewe kama ngoma. Mkewe alipochoka na kichapo, alirudi kwao mashambani.

“Jamaa alifurahia hatua ya mkewe na hata akampa nauli. Mke alifunganya kilichokuwa chake na kurudi kwao mashambani,” alisema mdokezi.

Baada ya miezi mitatu, jamaa alitoka kazini na kumkuta mkewe kwenye roshani akipiga gumzo na wanawake wenzake.
“Wewe ni nani aliyekuleta hapa? Si nilikupa nauli ukarudi kwenu, umekuja kufuata nini? Naomba uondoke, sitaki kukuona hapa kwangu!” jamaa alimfokea mkewe.

“Wewe hapo ulipo wajua kumtunza mke? Kula, kunywa na kuvaa ujue wapi? Ulinitesa kwa njaa, sasa nimepata mume mwenzako, ananitunza kama malkia. Kwako hutaniona ng’oo! Utasubiri sana,” kipusa alimjibu jamaa kwa bezo.

Jamaa alifanya uchunguzi kutaka kujua ni nani aliyemleta mkewe na kidudu mtu alimweleza ni jirani yake aliyejishindia mwanadada huyo.

Aliposikia hayo jamaa alienda kwa landilodi na kumwambia amrejeshee deposit yake atafute nyumba kwingine.
Alisema asingeishi na mume mwenza katika ploti moja. Alisema ingemuuma kumuona mkewe akiingia na kutoka kwa jirani.

Landilodi alimuomba jamaa ampe muda wa wiki moja amrejeshee pesa zake. Landilodi pia alimuunga jamaa mkono akimwambia kisa hicho ni cha aibu.