Kalameni ashambuliwa na kisura kwa kununulia rafiki keki

Na TOBBIE WEKESA

Imepakiwa - Wednesday, May 24  2017 at  15:20

Kwa Muhtasari

KENYATTA UNIVERSITY, NAIROBI

KIOJA kilizuka katika chuo hiki baada ya polo kushambuliwa na mrembo kwa kumnunulia rafiki yake keki siku yake ya kuzaliwa.

 

Inasemekana wawili hawa ambao ni wapenzi, walikutana kwa rafiki yao mmoja aliyekuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa iliyokuwa ikifanyika chuoni humu.

Kulingana na mdokezi, mrembo alishangazwa na zawadi aliyokuwa amenunua polo. Inasemekana polo alikuwa amenunua keki ya kifahari sana. Kwa upande wake, mrembo alikuwa amekuja mikono mikavu.

Duru zinasema baada ya kuitazama keki hiyo kwa muda, mrembo aliamua kumuuliza polo iwapo ni yeye alikuwa ameinunua.

Inadaiwa kuwa polo alimueleza mpenzi wake kuwa aliamua kumnunulia keki kama rafiki yake wa karibu. “Wewe unajua tu vizuri huyu demu hana mchumba wa kugharimia bethdei yake. Aliniomba nimsaidie,” polo alisema.

“Babe, juzi nilikiwa na bethdei, ulininunulia zawadi ya aina gani? Mbona pia hukuninunulia keki kama hii? Ungejua vile siku hiyo niliaibika,” mrembo alianza kumkaripia polo.

Inasemekana mrembo alianza kumhesabia polo makosa aliyomfanyia tangu waanze kuchumbiana. “Hakuna haja ya kuleta fujo hapa. Acha tupange siku nije tusuluhishe mambo,” polo alimrai mrembo.

Hata hivyo kipusa alimuonya polo dhidi ya kukanyaga kwake. “Ndio nimegundua sasa hunipendi. Kwangu usikanyage hata kidogo. Mapenzi yetu acha yaishe leo. Endelea kumpenda huyu kwanza,” kipusa alimueleza polo huku akiondoka karamuni.

Polo alijaribu kumzuia mrembo asiondoke lakini akamchapa kofi. “Huyu demu ni mimi nilikutambulisha kwake. Iweje leo unadai kumpenda kuliko mimi? Endeleeni na yeye,” mrembo alidai huku akiondoka.