Kidosho mwizi wa penzi plotini afurushwa

Imepakiwa Monday May 29 2017 | Na KIMANI wa NJUGUNA

Kwa Muhtasari:

RUIRU, KIAMBU

KIZAAZAA kilizuka hapa wanawake walipoungana na kumtimua mwanadada mmoja wakimlaumu kwa kuwanyakua wanaume wa wenyewe.

Penyenye zinasema haikuwa mara ya kwanza mwanadada huyo kulaumiwa kwa kuwanyemelea wanaume.

“Alikuwa ameolewa lakini kwa sababu ya tabia yake, alifukuzwa na mume wake na akahamia hapa,” alisema mdokezi.

Kulingana na mdokezi huyo, mwanadada huyo amejaliwa umbo na sura nzuri ambayo inadaiwa amekuwa akiitumia kuwachota wanaume wapendao uroda na kuzini nao.

“Mara tu alipohamia hapa na kupangisha nyumba yake ya kuishi, aliendelea na tabia yake ya kupenda maisha ya anasa na kuwatongoza wanaume,” alieleza mdokezi.

Kilichowaudhi wanawake wa hapa ni kuwamezea mate wanaume ambao wameoa.

Siku ya tukio, mwanamume mmoja ambaye ni jirani wa mwanadada huyo alikosa kufika kwake na vile vile, kidosho huyo hakurudi kulala kwake siku hiyo.

Ni kwa sababu hiyo mke wa jirani huyo alishuku kwamba mumewe alikuwa akijivinjari na mwanadada huyo.

Inasemekana kuwa alimshtaki mwanadada huyo kwa majirani akidai alitoweka na mumewe na alipowasili asubuhi, aliwapata majirani hao wakimngojea.

Walivamia kwake wakimlaumu kwa kuwapagawisha kimapenzi waume zao hadi wakasahau familia zao. “Kamwe hatuwezi kukubali uharibu familia zetu kwa ndumba zako tukinyamaza na leo hii utatambua sisi ni nani,” alifoka mwanamke mmoja na kuungwa mkono na wenzake.

Wanawake hao walitisha kumshambulia mwanamke huyo kabla ya kumfurusha kutoka hili. Hata hivyo, mwanamke huyo alidai hakuwa na uhusiano wa kimapenzi na mume wa mtu na kuwalaumu wanawake hao kwa kushindwa kukidhi wanaume wao kimapenzi.

Share Bookmark Print

Rating