Kioja wasanii wawili kupigania steji ya magari

Imepakiwa Sunday May 21 2017 | Na CORNELIUS MUTISYA

Kwa Muhtasari:

MACHAKOS MJINI

WAKAZI wa mji huu juzi waliwaonya wasanii wawili walio na mazoea ya kuzozania sehemu ya kituo cha magari wanayotumia kuwatumbuiza mashabiki.

Kulingana na mdokezi, msanii mmoja ambaye kwa kawaida huwa anatumbuiza wananchi katika steji ya magari mjini hapa alikosa kufika kwa wakati na msanii mwingine alipofika alianza kutumbuiza hadhira.

Penyenye zaarifu kuwa, ilipotimu saa tano hivi za asubuhi, msanii wa pili alifika katika uwanja huo akiandamana na kikosi chake na akapata uwanja umechukuliwa na msanii mwingine.

Alipandwa na hasira za mkizi na kuanza kumtusi mwenzake huku akimlaumu kwa kuingilia himaya yake ya kutumbuiza mashabiki na kuuza kanda zake.

“Nimekuwa nikitumbuiza wananchi kwa miaka mingi hapa. Mbona sasa umeanza kuniingilia?’’ alilalamika msanii huyo.

Inasemekana kwamba, msanii wa kwanza alianza kujitetea akisema kwamba hakuwa na nia mbaya kwa kuhubiria injili katika uwanja huo maana hata naye alikuwa na haki ya kufanya hivyo kwa sababu alikuwa amelipa ada inayostahili.

Hapo ndipo msanii wa pili alipomparamia mwenzake mithili ya simba marara na kumkwaruza kwa kucha zake usoni kabla ya wakazi kuingilia kati ya kuwatenganisha kisha wakawaonya wakome kuzozania uwanja kila mara.

Share Bookmark Print

Rating