Kipusa adai malipo kwa kuishi na jombi

Imepakiwa Sunday May 21 2017 | Na TOBBIE WEKESA

Kwa Muhtasari:

SIRISIA, BUNGOMA

WENYEJI wa eneo hili walibahatika kutazama sinema ya bure kipusa alipomlazimisha polo kumlipa fidia kwa muda aliokaa naye.

Inasemekana kipusa alikasirishwa na hatua ya polo ya kumuoa mke wa pili licha ya kukaa naye kwa miaka mingi.

“Nimevumilia kukaa na wewe miaka hiyo yote kwa taabu nyingi na mambo yanapoanza kuwa mazuri, unaamua kuoa mke mwingine. Wewe ni mwanamume wa aina gani? Ukora ndio mimi sipendi,” kipusa alimkaripia polo.

Penyenye zinasema polo alikuwa amepanga kuoa mke wa pili kwa siri.

Wakati haya yote yakifanyika, duru zinaarifu polo alikuwa ametulia tu bila wasiwasi wowote. “Mimi ninarudi kwetu. Tulipooana haukuwa hivi. Nimekulisha na kukulinda kama mtoto mdogo. Watoto wawili nimekuzalia. Lazima unilipe muda huo wote nimeishi na wewe,” kipusa alimueleza polo.

Inadaiwa kuwa polo aliposikia neno kulipa, alipigwa na butaa. “Eti nikulipe nini? Nani amekufuza hapa?” alimuuliza kipusa.

Inasemekana kipusa alianza kumhesabia polo mambo yote aliyomfanyia na kudai malipo.

Inadaiwa kipusa alianza kuvipanga vitu vyote alivyodai alivinunua. “Acha nikwambie hii nyumba tulipooana ilikuwa na godoro peke yake. Hivi vyote ni mimi nilinunua kwa jasho langu. Naenda navyo,” kipusa alimueleza polo.

Duru zinasema polo alianza kujitetea lakini maji yalikuwa yameshamwagika. “Kabla sijaondoka hapa, lazima utoe fidia ya miaka yote nimeishi nawe,” kipusa alimshurutisha jamaa.

Kulingana na mdokezi, majirani wa polo walibaki kutazama tu sinema kwa mbali.Inasemekana kipusa alimpa polo muda wa saa tatu awe ametoa hela alizohitaji kama fidia.

Share Bookmark Print

Rating