Kisura atimua dadake kwa kunyemelea mumewe

Imepakiwa Monday November 6 2017 | Na EDISON WANGA

Kwa Muhtasari:

KIEMBENI, MOMBASA

Kipusa aliyeolewa na mzungu mjini hapa alimtimua dada yake aliyekuwa akiishi naye akidai alikuwa na njama za kumnyemelea mumewe. Kipusa huyo alianza kwa kushuku tabia ya dada yake ya  kuvalia nguo fupi fupi.

Inasemekana mwanadada huyo alipoanza kuishi na dadake, alikuwa akivalia nadhifu lakini baada ya miezi mitatu, mambo yalibadilika akaanza kuvalia sketi fupi, suruali za kubana na blauzi fupi zilizoacha mgongo ukiwa wazi hadi kamba za sidiria zikawa zaonekana waziwazi.

Juhudi za kipusa kumkataza dadake ziliambulia patupu. “Hizi nguo za aibu aibu usizivalie hapa kwangu. Usidanganyike eti wanaume watakupenda na upuzi wote unaovaa.

Watafanya kukutamani tu bali hawatakupenda. Watakutumia na kukutupa kama masimbi,” kipusa alimweleza dadake. Kulingana na mdokezi, binti alimjibu dada yake kwa madharau akimwambia alikuwa na uhuru wa kuvaa apendavyo.

“It’s my dress my choice, huwezi kunizuia kuvaa ninavyotaka mimi. Heri nipendeze roho yangu,” alijibu kwa kiburi na kejeli.

Hali iliendelea hivyo hadi kipusa akaja kugundua dada yake alivalia hivyo kwa nia ya kumnasa mumewe kimahaba. Ilibidi azibe ufa badala ya kujenga ukuta.

Aliamua kutumia ujanja kumtimua. Alimwambia kwamba alipanga safari na mumewe kwenda ng’ambo. “Chukuwa vitu hivi umpelekee mama. Pamoja na hizi pesa. Mimi na mume wangu tunasafiri juma lijalo. Nikirudi nitakuarifu,” kipusa huyo alimweleza dada yake.

Kulingana na mdokezi wetu, inasemekana dada huyo hakurudi tena. Haikujulikana ikiwa hofu ya mwanadada ya kupokonywa mumewe na dada yake ilikuwa ya kweli au la, japo alisikika akisema hatakaribisha mwanamke mwingine kwake tena.

Share Bookmark Print

Rating