Mapolo wazuia pasta akijisaidia kwenye choo cha klabu

Na JOHN MUSYOKI

Imepakiwa - Monday, October 2  2017 at  12:48

Kwa Muhtasari

Kyondoni, MASINGA

WALEVI kutoka sehemu hii, walishangaza wengi walipomzuia pasta kuingia kwenye choo cha kilabu kwa haja ndogo.

 

Duru zinasema kuwa pasta alikuwa akipita karibu na kilabu hiyo lakini akakazwa na haja na akaamua kuingia msalani.

Makalameni waliokuwa wakinywa pombe walipomuona akikaribia, walianza kumrushia maneno na kumwambia asiingie kwenye choo hicho.

“Wewe pasta unaenda wapi? Nani alikuambia kuwa choo hiki ni cha kanisa? Unataka nini hapa? Kama unataka kukojoa nenda mahali pengine,” makalameni walisema.

Hata hivyo, mtu wa mungu alisisitiza kuwa alikuwa amekazwa lakini walevi hao hawakujali mbali waliendelea kumfukuza .

“Hakuna shida yoyote mimi kuingia kwenye choo. Nimekazwa sana na hakuna haja kuninyima nafasi ya kujisaidia. Hapa hakuna pahali pengine ambapo ningeendakujisaidia,” pasta alieleza.

Makalameni walizidi kuzua fujo huku wakitaka pasta aondoke kwenye choo cha kilabu.

Inasemekana pasta hakuwa na lingine la kufanya ila kuondoka kwa sababu walevi hao walikataa katakata kumruhusu kuingia chooni. Haikujulikana iwapo pasta alifaulu kupata pa kwenda haja.