Marafiki watibuana sababu ya kidosho

Na JOHN MUSYOKI

Imepakiwa - Wednesday, November 15  2017 at  10:45

Kwa Muhtasari

Kamandio, Kitui

URAFIKI wa makalameni waliokuwa wakiishi katika chumba cha kupanga sehemu hii ulifikia kikomo waliporushiana makonde wakizozania demu mgeni katika ploti.

 

Inasemekana wawili hao walianza kuzozana huku mmoja akimlaumu mwenzake kwa kumpiku kuwahi kichuna huyo aliyehamia plotini siku chache zilizopita. Mzozo ulianza chumbani walichokuwa wakiishi jamaa akimlaumu mwenzake kwa kumnyemelea mwanadada huyo.

“Haujui huyo ni mrembo wangu. Mbona unajaribu kunipima akili na unajua huyo ni mrembo wangu tangu aingie katika ploti hii? Usianze kunisumbua ama nikuonyeshe cha mtema kuni,” kalameni alisema.

Inasemekana jamaa kwa upande wake alimgeukia mwenzake na kumfokea vikali. “Wacha ufala jamaa. Demu huyu alikuja hapa na hakuna mmoja aliyekuwa anamjua. Wacha kujishasha eti huyu ni demu wako. Nina uhuru wa kumtongoza na hautakatiza mpango wangu,” kalameni alisema.

Ni katika purukushani hiyo wawili hao walipoanza kutwangana na kushtua wapangaji plotini. Baadhi ya wapangaji walionya makalameni hao dhidi ya kuzua zogo na kuvuruga amani. “Wanaume nyinyi hamna adabu kupigana kama wajinga. Kuna wanawake wengi kila mahali. Acheni ufala,” mpangaji mmoja alisema.

Kulingana na mdokezi, kichuna alidai kwamba alikuwa ameolewa na alikuwa na watoto wawili. “Yaani mnapigana kwa sababu yangu. Poleni sana. Mimi nimeolewa na nina mume na watoto wawili kwa hivyo acheni ujinga. Kila mtu ajipange na muache kunipigania,” demu alisema.

Inasemekana demu alipomwaga mtama makalameni walishangaa sana. Baadaye wawili hao walihama ploti hiyo na inasemekana kila mmoja alienda kukodi chumba chake. Haikujulikana ikiwa walisameheana baada ya uadui kuzuka kwenye tukio hilo.