Mimba ni yangu, polo apayuka kuzima harusi

Na  TOBBIE WEKESA

Imepakiwa - Thursday, November 2  2017 at  11:15

Kwa Muhtasari

BUTULA, BUSIA

Kalameni mmoja kutoka eneo hili aliwashangaza wengi aliposimamisha harusi akidai kwamba bi harusi alikuwa na mimba yake.

 

Kulingana na mdokezi, kalameni alipata ujumbe kutoka kwa rafiki yake mmoja kuwa mpenzi wake alikuwa akipanga kuelekea jijini na polo fulani.

Vilevile alimueleza kuwa kabla ya kuondoka, kulikuwa na mpango wa wao kufunga harusi kwanza. Duru zinasema kalameni alianza kufanya uchunguzi.

Inasemekana alipobaini kwamba ni ukweli mrembo wake alikuwa akipanga kufunga harusi na polo mwingine, aliamua kutulia hadi siku ya harusi yenyewe.

Siku ilipowadia, kalameni hata hakungojea pasta aulize wale waliopinga harusi wajitokeze. Kalameni aliinuka kutoka kwenye kiti na kumrai pasta asimamishe harusi.

“Pasta nakuheshimu sana lakini nakuomba usimamishe hii harusi,” kalameni alimrai pasta. Pasta alibaki ameduwaa asijue la kufanya. “Huyu msichana alikuwa mpenzi wangu.

Kwa sasa ana mimba yangu. Kama mnataka kuendelea na harusi basi tusikilizane atakapojifungua aniletee mtoto wangu,” kalameni alimueleza pasta.

Duru zinasema pasta alibaki mdomo wazi. Kalameni aliketi huku waliohudhuria harusi wakishangaa. Penyenye zinasema polo aliyekuwa akifanya harusi na mrembo alikuwa ametoka tu jijini. Alielekea kwa akina mrembo na kumzuzua kwa hela alizokuwa nazo.

Inasemekana alipoona hela za polo, mrembo aliamua kubadilisha penzi lake. Duru zinaarifu kipusa alianza kuhepa simu za mpenzi wake wa hapo awali.

“Nataka kila mtu ajue hivi, nimegharamika sana kumtunza huyu msichana. Mara kwa mara alikuwa akija kwangu. Hadi tukasikilizana tupate mtoto. Mimi ninataka mtoto wangu,” kalameni alisisitiza. Ilibidi pasta asimamishe uchaguzi.