Mke taabani kwa kukosa kuandaa busaa Krismasi

Na TOBBIE WEKESA

Imepakiwa - Thursday, December 28  2017 at  20:36

Kwa Muhtasari

KOTUR, TESO

WENYEJI wa eneo hili walipigwa na butwaa polo alipomzomea vikali mke wake kwa kukosa kuandaa busaa ya Krismasi.

 

Kulingana na mdokezi, polo alikuwa akitarajia kipusa amuandalie busaa. Alishangaa sana alipogundua kwamba kipusa hakumuandalia kinywaji chake ambacho anakienzi sana.

Inasemekana polo alikuwa akiandaliwa busaa na mkewe kwa miaka mingi. Duru zinasema siku ya Krismasi ilipofika, polo alimueleza mkewe kwamba marafiki zake wangejumuika naye jioni. Polo alimuelekeza mkewe ajitayarishe kuwandalia busaa.

“Mara hii sijaunda busaa. Hao marafiki zako nitawapikia chai,” kipusa alimueleza polo. Inadaiwa polo alimuangalia kipusa na kunyamaza kwa dakika tatu. “Wewe ni kama umepagawa. Hujui unalosema. Krismasi bila busaa si Krismasi. Wageni wangu wanakuja jioni na ni lazima wanywe busaa,” polo alisema kwa ukali.

Kipusa alimlaumu polo kwa kumkanganya kwani hapo awali polo alikuwa amedai kuachana na busaa.

“Wewe uliniambia mambo ya busaa umeachana nayo. Ulitaka nitengezee nani anywe? Isitoshe nimetoka kwetu nikiwa nimechelewa. Sikuwa na wakati,” kipusa alijibu.

Polo alianza kumzomea mkewe huku akiapa kumpa adabu.
“Mimi sikukuambia nimeacha kabisa. Ni kupunguza tu. Isitoshe Krismasi ni sherehe kubwa sana. Utaacha uvivu,” polo alimzomea mkewe huku akitishia kumtimua.

“Mimi sitaki mtu wa kuniletea aibu hapa. Bila busaa hutakaa hapa. Uliona kwenu ni kuzuri kushinda kwangu,” polo alimzomea mkewe.

Majirani wa polo walianza kukusanyika pembezoni kutazamia sinema ya bure. “Wanawake wote kijijini humu walienda kwao na wakarudi kwa wakati kuandalia waume zao krisimasi ya kukata na shoka. Wewe je?” polo alizidi kufoka. Kipusa aliamua kunyamaza.

“Sijawahi ona sherehe ovyo kama hii kwangu. Maandalizi yamekuwa duni kabisa. Na ni wewe umekuwa sababu,” polo alimzomea kipusa.