Mpishi wa hoteli akutwa ameficha mahamri kwa suruali

Imepakiwa Thursday November 2 2017 | Na JOHN MUSYOKI

Kwa Muhtasari:

KYONDONI, MACHAKOS

KALAMENI mmoja kutoka sehemu hii alikiona cha mtema kuni alipofumaniwa na mwenye hoteli jikoni akiwa ameficha mahamri kwenye mifuko ya suruali yake.

Inasemekana kalameni alikuwa mpishi hoteli hiyo lakini alikuwa mlafi. Siku ya kioja kalameni alijipata kona mbaya alipofumaniwa na mwenye hoteli hiyo jikoni akiendelea kutafuna mahamri huku akiyatoa kwenye mfuko wake wa suruali.

Mwenye hoteli kwa hamaki alianza kumfokea jamaa.

“Yaani ni wewe huiba mahamri yangu? Kuanzia leo tamaa yako imefikia kikomo. Hautawahi kutafuna mahamri yangu tena,” mdosi alimkemea kalameni na kumwangushia kofi moto usoni.

Kalameni alipiga nduru zilizovutia waliokuwa karibu lakini hakuna aliyemtetea kwa sababu wengi walidai jamaa alikuwa mwenye tamaa sana na alikuwa akila chakula bila ruhusa.

“Wacha fisi afunzwe funzo. Nilimuonya siku nyingi aache kula mahamri ya boss lakini alikataa ushauri wangu, leo amepatikana, wacha atwangwe,” weita alisikika akiarifu wenzake huku vita vikichacha jikoni.

“Leo utalala polisi kwa sababu umeniudhi sana na kuharibu biashara yangu,” mdosi aliwaka.

Ni katika hali hiyo kalameni alipopata nafasi nzuri ya kuchomoka aliposikia kuwa angepelekwa polisi.

Share Bookmark Print

Rating