Mzee wa kanisa ajuta kuonja tunda haramu

Imepakiwa Wednesday May 17 2017 | Na LEAH MAKENA

Kwa Muhtasari:

MACHAKOS MJINI

POLO wa hapa alipata aibu ya mwaka pale ilipobainika kuwa alivamiwa na kuadhibiwa baada ya kumfumaniwa akichovya asali kutoka mzinga wa mwanamume mwingine na wala hakuwa amepata ajali jinsi alivyodai.

Duru zasema kuwa jamaa huyo alikuwa mzee wa kanisa japo alikuwa akiwamezea mate akina dada licha ya kuwa na mke na watoto sita.

Inasemekana kuwa jamaa alianza kunyemelea mama mmoja kanisani ambaye mumewe alikuwa akifanya kazi mbali na nyumbani.

Minong’ono yasema kuwa wawili hao walianza kurushana roho kwenye lojing’i na baada ya muda mama alianza kumualika kwake nyumbani.

Kulingana na penyenye za mtaa, jirani mmoja alimpigia simu mume wa mwanamke huyo kumuarifu jinsi mkewe alivyokuwa akigawa asali. Hapo ndipo jamaa alipanga safari ya ghafla na kufika kwake usiku wa manane.

Yasemekana kuwa vuta nikuvute ilishuhudiwa pale mama alipodinda kufungua mlango. Hata hivyo, kwa kuhofia kuvutia umati, jamaa aliufungua na kuanza kumenyana na mwenye boma.

“Wawili hao walimenyana nusura mla vya watu auawe baada ya kukabwa koo lakini alinusurika na kuponyoka akiwa na majeraha mabaya yaliyomlazimu kulazwa hospitali kwa muda,” alisema mdokezi.

Polo alikuwa akihadaa washiriki waliofika hospitalini kumjulia hali kwa mara ya kwanza kuwa alivamiwa na wakora. Hata hivyo, mambo yalianikwa wazi mume wa mama huyo alipowaelezea washiriki jinsi alivyompata jamaa huyo akila uroda na mkewe katika kitanda chao cha ndoa.

Inasemekana baada ya kupona, jamaa hakukanyaga kanisani huku mke aliyezini naye akiamua kurudi kwa wazazi wake katika kaunti jirani.

Share Bookmark Print

Rating