Pasta afumaniwa akimchuna ngozi kondoo wake

Na CORNELIUS MUTISYA

Imepakiwa - Thursday, August 4  2016 at  07:44

Kwa Muhtasari

KISSONI, Machakos

Mhubiri wa kanisa moja eneo hili alipokezwa kichapo cha mbwa koko na wakazi alipofumaniwa akirushana roho na mke wa muumini wa kanisa lake katika chumba chake kanisani.

 

PASTA wa kanisa moja eneo hili alipokezwa kichapo cha mbwa koko na wakazi alipofumaniwa akirushana roho na mke wa muumini wa kanisa lake katika chumba chake kanisani.


Kulingana na mdokezi, pasta alihamishiwa kanisa hilo mwaka uliopita. Staili zake za mahubiri na mienendo yake ziliwatia hofu waumini mpaka baadhi yao wakaanza kususia ibada. Licha ya waumini kulalamika kuhusu hulka zake, hakuna hatua yoyote ya kinidhamu aliyochukuliwa na wakubwa wake.


“Pasta aliondokea kuwa na tabia potovu. Alikuwa akiwatongoza akina mama kanisani bila kuogopa chochote,’’ alisema mdokezi.


Penyenye za mtaa zaarifu kuwa, pasta alianza uhusiano wa kimapenzi na mama mmoja. Mapenzi yao yalivuma mno mpaka mumewe akapata habari akiwa jijini Nairobi anakochapa kazi. Aliamua kuajiri 'makachero’ wa kuchunguza nyendo za pasta na mkewe ili akiwafumania, awafunze adabu ya mwaka.


Siku ya tukio, Pasta alimpigia simu mama huyo mwendo wa saa mbili unusu usiku akimtaka amletee maji chumbani mwake. Mama alifika akiwa na mtungi wa maji na akajibanza kwa kiti sebuleni. Baadaye walijitoma katika chumba cha kulala na kujibanza kitandani ambako walianza kurushana roho.


Inasemekana kwamba walipokuwa wamezama katika shughuli zao, 'makachero’ , walimpigia simu mume wa mwanamke huyo na akafika mara moja.


Kulingana na mdokezi, mke wa polo alitoroka kupitia dirishani mambo yalipochacha na kumuacha pasta akitandikwa vikali. Hata hivyo, aliokolewa na maafisa wa usalama waliokuwa kwenye doria.


Duru zaarifu kuwa, polo alisikika akiapa hatamkubali mkewe tena kwa sababu ya uzinzi.