Pasta amramba kofi muumini mpenda anasa kwa kusinzia

Na KIMANI wa NJUGUNA

Imepakiwa - Tuesday, May 30  2017 at  15:31

Kwa Muhtasari

MWEA, KIRINYAGA

KASISI wa kanisa moja eneo hili aliwaacha wafuasi vinywa wazi alipomtimua muumini aliyesinzia alipokuwa akihubiri neno la Mungu.

 

“Kalameni aliyehusika anajulikana kwa kupenda anasa za kila aina na hasa ulevi wa kupindukia,” alisema mdokezi. Mkewe kalameni ni mcha Mungu na kiongozi wa kanisa na wazee walisisitiza ni lazima mumewe awe akihudhuria ibada kwa sababu ya cheo cha mkewe.

“Jamaa hangetaka mke wake akose cheo na akaamua kuwa akiandamana naye kanisani,” akaeleza mdokezi. Hata hivyo, jamaa alijipata kwenye kibarua kigumu kwani aliendelea kushiriki burudani vilabuni na kumfanya awe akisinzia kanisani Ibada ikiendelea.

Jamaa alihudhuria tamasha la burudani lililoporomoshwa na msanii marufu eneo hili hadi chee, alisimulia mdokezi.

Na siku iliyofuata walipohudhuria ibada, jamaa alikuwa mchovu na akalala fo fo fo na kuanza kukoroma jambo lililomfanya kasisi kukasirika. Inasemekana pasta alimuendea na kumzaba kofi lililomwamsha kalameni.

“Ikiwa unadhani kanisa ni chumba cha kulala ukichoka na kuhudumia Serrano jua kwamba mimi sivumilii upuzi kama huo,” alichemka mhubiri.

Jambo lililowashangaza waumini ni kwamba kasisi huyo alimtimua kalameni na kumuonya dhidi kukanyaga kanisani akiwa ametoka kuhudumia shetani.

Penyenye zinasema mke wa jamaa na baadhi ya waumini hawakufurahishwa na kitendo cha pasta na wakaondoka kanisani wakiteta.

Walimlaumu pasta kwa kushindwa katika kazi yake ya kuwalea waumini kiroho na kugeukia nguvu za mwili kuwakosoa.

Kikao cha wazee wa kanisa kiliandaliwa na pasta akaonywa vikali kurekebisha tabia au achukuliwe hatua za kinidhamu.