Polo achemka kisura kumrushia mistari

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Thursday, May 18  2017 at  18:04

Kwa Muhtasari

KIAMBU ROAD, KIAMBU

SINEMA ya bure ilishuhudiwa kwenye basi linalohudumu barabara hii kalameni alipozusha akiteta kuwa kimwana aliyeketi kando yake alikuwa akimkatia ilhali ana mke.

 

Yasemekana jamaa aliabiri matatu hiyo jijini Nairobi kuelekea Kiambu naye kidosho aliingia baadaye kidogo na kuketi kando yake.

Duru zaarifu kwamba gari hilo lilipojaa na kuanza safari, mwanadada alivunja kimya kwa kumsalimia jamaa, “Umeshindaje baba? Umevalia nadhifu kweli,” kidosho alianza.

“Nimeshinda salama nashukuru,” mzee alijibu. Kulingana na mdokezi, mwanadada huyo aliendelea kuongea huku kalameni akionekana kutotaka mazungumzo.

“Inaonekana una mke anayekujali mzee. Hata hivyo, nikipata fursa ya kuolewa nitamjali mume wangu ili asiwe na mpango wa kando. Hata wewe naweza kukufanyia makuu na matamu,” kipusa alimweleza jamaa akimgusa mikono.

“Hei, kwani hili gari huwa mnabeba abiria wa aina gani wasiowapa abiria wengine amani?” jamaa alifoka.

“Huyu mwanamke amekuwa akinizungumzia tangu nilipoingia na anaonekana kuwa na mambo mengine, hajui mimi nina mke na watoto?” aliwaka kila mmoja akionekana kushangazwa na tukio hilo.

Inasemekana jamaa alichemka akisema kuwa yeye ni mzee wa kanisa aliyeheshimika kanisani na kijijini. “Mimi nina heshima zangu si tu kijijini bali pia kanisani.

Wewe mwanadada unanichukulia vipi ukisema niwe mpango wako wa kando?” kalameni alipaza sauti. Mwanadada huyo aliaibika kiasi kwamba alilazimika kushuka.

“Kweli kuna watu wasio na adabu, yaani amekosa mume aanze kunyemelea waume wa wengine?” aliuliza mama mmoja na kusababisha abiria wote kuangua kicheko.