Akamatwa akiruka ua wa jirani usiku

Imepakiwa Thursday February 4 2016 | Na MWANDISHI WETU

Kwa Muhtasari:

Siku ya arobaini ilifika kwa polo wa eneo hili la Makongeni, Thika alipokamatwa akijaribu kuruka ua kuingia kwa jirani kuwanyemelea mabinti usiku.

MAKONGENI, Thika

SIKU ya arobaini ilifika kwa polo wa eneo hili la Makongeni, Thika alipokamatwa akijaribu kuruka ua kuingia kwa jirani kuwanyemelea mabinti usiku.

Kulingana na mdokezi, jirani ya polo alikuwa akilalamika kwamba kulikuwa na mtu aliyekuwa akiingia kwake wakati wa usiku na kuwaita binti zake kwa majina.

“Kila usiku, huwa ninasikia sauti ya mtu ikiitana nje ya nyumba. Huyo mtu huwa ni nani?” mwenye boma aliwauliza binti zake.

Inasemekana vipusa hao walimwambia baba yao kwamba pia wao walikuwa wakisikia sauti za mtu huyo.

“Dadi hata sisi humsikia tu. Lakini hatumjui,” mabinti walimjibu baba yao.

“Leo lazima atarudi na atanipata. Na sijui yeye hupita wapi,” mzee alisema huku akiapa kumnasa jombi huyo.

Inasemekana kuwa aliamua kumwekea polo mtego kwa kujificha kando ya ua la nyumba yake.

“Saa za polo kuruka ua zilipofika alikunja suruali yake tayari kupanda ua la boma ya jirani yake bila kujua alikuwa amewekewa mtego. Kabla ya polo kuruka upande ule mwingine, alikamatwa na mwenye boma,” alisimulia mdokezi.

Mbona wanyemelea wanangu?

“Kwani ni wewe? Mbona unawanyemelea wasichana wangu? Mbona usiwaongojee huko nje mchana badala ya kuwanyemelea usiku?” mzee alimkaripia polo.

“Haki nisamehe, huwa ninatamani kuzungumza nao,” polo alijitetea lakini mzee aliendelea kumkaripia. “Nilikuwa nikifikiria kuwa wewe ni jirani mwema. Kumbe kikulacho ki nguoni mwako. Una bahati sana. Ningekumaliza saa hizi,” mzee alimweleza polo .

Inasemekana kuwa mzee aliwaita binti zake kumuona mgeni wao wa kila usiku.

“Potea hapa kabisa. Siku nyingine nikikuona kwa hili boma langu hata kama ni mchana, utakiona,” mzee alimweleza polo ambaye alitimka mbio bila kuangalia nyuma.

Share Bookmark Print

Rating