Atoroka nyumbani kuhepa kulipa karo

Na GRACE KARANJA

Imepakiwa - Saturday, January 9  2016 at  17:35

Kwa Muhtasari

Kalameni kutoka mtaa huu wa Dandora, Nairobi ameshangaza wakazi kwa kutoroka nyumbani katika kile ambacho mkewe alisema ni kuhofia kumlipia mwanawe karo ya shule ya upili.

 

DANDORA, Nairobi

KALAMENI kutoka mtaa huu wa Dandora, Nairobi ameshangaza wakazi kwa kutoroka nyumbani katika kile ambacho mkewe alisema ni kuhofia kumlipia mwanawe karo ya shule ya upili.

Kulingana na mdokezi, jamaa huyo alikuwa amemwonya mkewe dhidi ya kumwitisha karo ya shule ya upili akisema maisha ni magumu.

“Kila mara alikuwa akimwambia mkewe kwamba angehepa asipopata kazi aweze kulipa karo,” mdokezi alisema.

Inasemekana kwamba matokeo ya mtihani wa darasa la nane yalipotangazwa, alifahamishwa kwamba mwanawe alipata alama za juu na alikuwa miongoni mwa wale waliofanya vyema zaidi.

Siku iliyofuata, jamaa aliamka mapema na kupakia nguo zake kwenye mkoba mkubwa kisha akamwita mkewe.

“Ninakumbuka vizuri kabla ya mwaka jana kuisha nilikwambia kwamba endapo sitakuwa nimepata kazi itakayoniwezesha kumlipia mtoto karo ya shule nitaondoka hapa. Sasa ninaona wakati umefika. Kama una lolote la kuniambia sema muda wangu unayoyoma,” jamaa alimwambia mkewe.

Kupambana na maisha

Hata hivyo, mkewe alimwambia kwamba alichukua hatua ambayo haikufaa na badala yake angepambana na maisha kama wanaume wengine.

“Sasa unataka niwaambie watoto nini? Mbona usipambane na maisha kama wanaume wengine mtaani?” mke akauliza.

Inasemekana maneno ya mkewe yalimwongeza jamaa huyo uchungu moyoni hivi kwamba alitaka kumchapa.

“Endelea kupambana hata wewe, mimi sitajiaibisha mbele ya mwanangu nikimweleza hadithi eti nimekosa karo yake. Utajua utakayowaeleza,” buda alimjibu mke wake na kuchukua mkoba na kuondoka.

Kulingana na mdokezi, mkewe alipowapigia simu wakwe zake ili kujua kama mumewe alienda mashambani alifahamishwa kwamba hawakuwa wamemwona na kufikia wakati wa kuandika habari hizi hakuna aliyejua alikokuwa.

Familia iliandaa kikao na ikaamuliwa akikosa kupatikana, wangepiga ripoti kwa polisi.