Demu azirai kupata baba mkwe lojing'i

Na KIMANI wa NJUGUNA

Imepakiwa - Wednesday, January 13  2016 at  10:14

Kwa Muhtasari

Mwanadada mmoja wa Kiambu Mjini alipoteza fahamu na kuanguka alipoingia ndani ya lojing’i kushiriki mipango ya kando na kumpata baba mkwe akiwa bawabu wa gesti hiyo.

 

MWANADADA mmoja wa Kiambu Mjini alipoteza fahamu na kuanguka alipoingia ndani ya lojing’i kushiriki mipango ya kando na kumpata baba mkwe akiwa bawabu wa gesti hiyo.

“Mwanadada huyo aliolewa miaka mitano iliyopita na jamaa ambaye alikuwa akifanya kazi katika kampuni moja jijini Nairobi na wakabarikiwa na watoto wawili,” akaeleza mdokezi.

Inasemekana jamaa aliangukiwa na bahati alipopata kazi ng’ambo na akamuacha mkewe nchini. Kulingana na mdokezi, jamaa alikuwa akimtumia mkewe pesa za kutosha kuwatunza watoto.

“Baada ya muda, mwanamke huyo alianza kuhisi upweke na kiu cha uroda kwa sababu hakuna mwanamume ambaye alimrushia ndoano,” akaendelea mdokezi.

Ni wakati huo ambapo alikata kauli kutongoza wanamume na akampata barobaro mmoja aliyemaliza kidato cha nne mwaka jana.

Bila kupoteza muda, mwanamke huyo alianza kumtumia arafa moto moto za kimapenzi kijana huyo.

Isitoshe, alimzuzua chali huyo kwa kumtumia pesa za matumizi yake.

Siku ya kisanga, wawili hao walipanga kukutana katika hoteli moja na baada ya mapochopocho na vileo, waliamua kujitoma kwenye lojing’i ili waburudishane faraghani.

Jukumu la kukodisha vyumba

Walielekea katika gesti moja na wakafahamishwa kwamba jukumu la kukodisha vyumba vya kulala lilikuwa la mlinzi wa usiku.

Mara tu alipochomoa pesa za kukodisha chumba na kugundua alikuwa anamkabidhi baba mkewe pesa hizo.

“Ala! Kwa hivyo, mwanangu alimuoa mwanamke ambaye anawalipa vijana wadogo wamburudishe kimapenzi? Tabia kama hii haitafanyika nikiwa hai na lazima nilinde heshima ya familia yangu,” alifoka mzee.

Alipomaliza tu kuzungumza, demu alianguka sakafuni kwa kishindo.

Alipewa huduma za kwanza na akapata fahamu, bawabu huyo aliinua rungu akitaka kumuangushia polo kichwani, lakini akahepa.

Kuona mambo yalikuwa yamepasuka, mwanadada huyo alichomoka kama mshale.

Iliwabidi waliokuwa karibu kumtuliza mzee huyo huku wakimlaumu mwanadada kwa tukio hilo.

Dondoo za Hapa na Pale ni visa vinavyojiri kila siku sehemu tofauti nchini na kimataifa. Tuma habari kwa:dondoo@ke.nationmedia.com/ taifa@ke.nationmedia.com au swahilihub@ke.nationmedia.com