Harusi 'bomba' ya rafike yafanya mlevi kuasi pombe

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Thursday, January 7  2016 at  11:41

Kwa Muhtasari

Kalameni aliwaacha wakazi wa hapa Kanyama, Karatina wakivunjika mbavu kwa kicheko alipotangaza hadharani nia yake ya kuacha mvinyo na kuoa.

 

KANYAMA, Karatina

KALAMENI aliwaacha wakazi wa hapa Kanyama, Karatina wakivunjika mbavu kwa kicheko alipotangaza hadharani nia yake ya kuacha mvinyo na kuoa.

Polo huyo ni rafiki wa karibu wa jamaa aliyefunga ndoa.

Yasemekana kalameni alikuwa mtumwa wa mvinyo kiasi kwamba alikuwa ameapa kutoasi useja.

“Marafiki zake walifahamu jamaa alikata kauli kutooa kulingana na msimamo wake wa hapo awali,” alieleza mdokezi wetu.

Penyenye zinaarifu kuwa wakati mmoja jombi alisikika akisema ameolewa na pombe.

“Ilikuwa miujiza kwa polo kubadilisha msimamo wake,” alisema mdokezi wetu.

Siku ya kioja jamaa aliungana na wengine kushuhudia rafiki yake akifunga pingu za maisha.

Harusi hiyo ilianza na kuendelea vyema.

Maharusi walitakiwa kila la heri wakianza ukurasa mpya wa maisha yao kama bwana na bibi.

Ulifikia muda wa jamaa na barafu yake ya roho kuvishana pete.

“Ninaomba kuunganisha hawa kuwa kitu kimoja maishani, kwa furaha na dhiki. Kwanza kabla ya hapo, iwapo kuna anayepinga uhalali wa ndoa hii ainue mkono na aeleze sababu zake,” alitangaza pasta aliyeongoza harusi hiyo.

Kalameni ainua mkono

Kalameni aliyeketi nyuma ya ukumbi aliinua mkono na kunyanyuka akielekea aliposimama pasta.

“Sijasimama kupinga ndoa hii, ila kutangaza malengo yangu ya huu mwaka. Nilikuwa mtumwa wa mvinyo na nimeacha kabisa. Mui huwa mwema, sasa niko njiani kuasi ukapera. Hakuna maisha matamu kama kupata mchumba. Huyu jamaa anayefunga pingu za maisha ni rafiki yangu na amenipa changamoto ya kuoa,” alisema jombi kwa ucheshi.

Bwana na bibi harusi walishindwa kuzuia kicheko.

Harusi hiyo iliendelea na maharusi waliunganishwa kwa furaha.

Yasemekana pasta huyo alialika kalameni kwenye ofisi yake ili wajadili mipango yake ya kuasi useja.