Jombi mpenda chupa ala viboko kutelekeza

Imepakiwa Wednesday February 3 2016 | Na SAMMY WAWERU

Kwa Muhtasari:

Buda wa hapa Ngandu, Nyeri alijuta baada ya kuchapwa vikali na mkewe kwa kukosa kufika mbele ya kikao cha wazee wa kijiji.

NGANDU, Nyeri

BUDA wa hapa Ngandu, Nyeri alijuta baada ya kuchapwa vikali na mkewe kwa kukosa kufika mbele ya kikao cha wazee wa kijiji.

Yasemekana jamaa huyo alikuwa amezembea katika kutelekeza majukumu kama mume na kiongozi wa familia yake.

“Mkewe ndiye aliyeachiwa majukumu yote ya familia,” mdokezi alieleza. Penyenye zasema jamaa alikuwa amezama kwenye mvinyo na mkewe alikuwa akilalamika kila mara.

“Mimi nimeolewa na pombe, wanawake hawana faida kwangu” kalameni alikuwa akisema akitoka kwa mama pima.

Mkewe alichoshwa na tabia ya mumewe akifahamu walikuwa na mtoto anayefaa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu.

Aliamua kumfikisha mbele ya kikao cha wazee wa kijiji. Jamaa alitumiwa ilani ya kufika barazani. Siku ya kikao, polo alirauka jogoo wa kwanza akiwika na kufahamisha mkewe kuwa angefika kikaoni.

Alifululiza hadi kwa mama pima ili kujiburudisha. Mkewe alijitayarisha na kuelekea kikaoni akitarajia mumewe angehudhuria.

Saa ziliyoyoma na dalili za jombi kuwasili hazikuonekana. Simu ya kalameni ilipopigwa, alikuwa ameizima. Mama huyo aliomba wazee hao ruhusa akamsake mumewe na akaelekea kwa mama pima ambapo alimpata jamaa akiwa mlevi chakari.

“Mwanamke ulidhani kunifikisha kwa wazee wa kijiji ndiyo dawa? Niachie raha zangu,” alifoka jombi.

Gumegume lacharazwa

Mkewe alighadhabishwa na matamshi ya gumegume lake ndiposa akaanza kulicharaza vilivyo.

“Leo utatambua mimi ni huyo mwanamke unayetaja. Utakuwa ukitekeleza majukumu yako bila kuelezwa,” alichemka mama huku akimcharaza. Marafiki wa jamaa walimuunga mama huyo.

“Asidhani akituona hapa huwa hatushughulikii familia zetu, maslahi ya familia kwanza, mengine baadaye,” alisema buda mmoja.

Haikufahamika mzozo wao ulifikia wapi polo alipoagizwa na wenzake kuondoka kwenda kushughulikia majukumu ya familia yake.

Share Bookmark Print

Rating