Makalameni wazima ulaghai wa mganga

Na TOBBIE WEKESA

Imepakiwa - Tuesday, March 15  2016 at  12:04

Kwa Muhtasari

Ujanja wa mganga mmoja wa eneo hili la Kitale ulifikia kikomo baada ya kuvamiwa na mapolo wawili kwa kuwalaghai Sh10,000 akidai angemtibu ndugu yao.

 

KITALE MJINI

UJANJA wa mganga mmoja wa eneo hili la Kitale ulifikia kikomo baada ya kuvamiwa na mapolo wawili kwa kuwalaghai Sh10,000 akidai angemtibu ndugu yao.

Inasemekana kuwa mganga alipokea pesa hizo akidai angemtibu ndugu ya mapolo hao ambaye alikuwa akiugua kwa muda mrefu.

Mganga aliwaeleza kwamba ndugu yao alikuwa amerogwa na kwamba wangemfahamu mtu aliyekuwa akimfanyia hivyo. Hata hivyo, licha ya hakikisho la mganga, hali ya mgonjwa iliendelea kuwa mbaya.

Kulingana na mdokezi wetu, mapolo wote walikubali kubuni mbinu itakayotumika kubaini ikiwa mganga huyo alikuwa na nguvu za kutibu.

“Waliamua kubuni kisa cha uongo ambapo walimuendea mganga huyo na kumweleza kuwa mwizi alivunja lango la supamaketi yao na kubeba pesa zote,” alieleza mdokezi.

Mganga alianza kupiga ramli huku akiwaita mababu zake waanze kufanya kazi. Inasemekana kuwa baada ya dakika chache, mganga alisitisha vituko vyake.

“Jinsi nilivyowaambia ugonjwa wa jamaa wenu na mtu ambaye kamfanyia hayo madhambi, ndio jinsi nitawataja wezi wa supamaketi yenu ni akina nani,” mganga aliwaeleza mapolo ambao walikuwa wametega sikio ndi kupata maneno ya mganga kwa ufasaha.

“Wezi walikuwa watano. Na hivyo vitu walichukua watarudisha baada ya siku tatu. Hao wezi hawatoki mbali. Wote ni majirani zenu,” mganga aliwaelezea mapolo.

Uwezo tunao?

“Mzee, leo tumejua siri yako. Wewe ukituangalia, tunaweza miliki supamaketi? Kama kujenga kibanda cha kuuza sukuma wiki hatuwezi, je supa nayo?” mapolo walimuuliza mganga.

“Nimesema Mungu akipenda, mtakuja jenga supamaketi,” mganga aliwaeleza mapolo huku akianza kutetemeka. 

“Tumejua kuwa wewe kazi yako ni kuwahadaa watu. Leo umevuliwa nguo hadharani. Pesa tulizokupa ili umtibu ndugu yetu weka hapa haraka,” mapolo walimuamrisha mganga huku wakimtoa ndani ya nyumba wakimzaba makofi bila huruma.