Mama azuia mwanawe kuoa muuza-baa mke wa pili

Imepakiwa Saturday April 2 2016 | Na CORNELIUS MUTISYA

Kwa Muhtasari:

Polo wa hapa Lita, Machakos alijipata katika njia panda pale jaribio lake la kuoa mke wa pili lilipotibuliwa na mama yake aliyetisha kumlaani.

LITA, Machakos

POLO wa hapa Lita, Machakos alijipata katika njia panda pale jaribio lake la kuoa mke wa pili lilipotibuliwa na mama yake aliyetisha kumlaani.

Kulingana na mdokezi, polo ambaye ameoa na kujaliwa watoto wanne alianzisha uhusiano wa kimahaba na mwanamke mwingine mhudumu wa baa.

Uhusiano wao ulimea mizizi na kujidhibiti mpaka wakaamua kufunga pingu za maisha.

Penyenye zaarifu kwamba, habari za mpango wao wa kuoana zilivuma kote mithili na wazaz, ndugu na marafiki wa polo huyo walipokea habari hizo hisia mseto.

Baadhi yao walimuunga mkono na wengine wakapinga vikali mipango yake.

“Azimio la polo kuoa mke wa pili lilipingwa vikali na wazazi na marafiki na kuungwa na ndugu zake. Wazazi walidai polo kuoa mke wa pili, tena mhudumu wa baa, ilikuwa ni kujiletea balaa,’’ akasema mdokezi.

Mama aapa kumlaani mwana

Inasemekana kwamba, mama ya polo aliposikia habari hizo aliapa kumlaani mwanawe endapo angeendelea na mpango wake na kuoa mke wa pili.

Siku ya tukio, polo alifika nyumbani akiandamana na mwanamke aliyenuia kuoa akikusudia kumjulisha rasmi kwa wazazi wake.

Hata hivyo, mama yake alipowaona, alianza kuwatupia cheche za matusi huku akitisha kumlaani polo.

“Nilikuzaa, nikakulea na kukusomesha. Tayari una mke na watoto wanne nyumbani. Mbona unatusaliti kwa kutaka kuoa mke wa pili, tena mhudumu wa baa?" mama alifoka huku akitisha kuvua nguo zake kwa hasira za mkizi.

Duru zaarifu kwamba, kwa kuchelea kukumbwa na laana za mama mzazi, polo aliamua kukatiza mpango wa kuoa mwanamke huyo, lakini shingo upande na akawaomba wazazi na mkewe msamaha.

Share Bookmark Print

Rating