Mwanadada pabaya kutumia pasta SMS ya mapenzi

Imepakiwa Tuesday February 9 2016 | Na CORNELIUS MUTISYA

Kwa Muhtasari:

Kizaazaa kilizuka eneo hili la Kauti, Kathiani mke wa pasta wa Kanisa moja alipojawa na hasira za mkizi na kumcharaza muumini wa kike kwa kumtumia mumewe arafa ya mapenzi.

KAUTI, Kathiani

KIZAAZAA kilizuka eneo hili la Kauti, Kathiani mke wa pasta wa Kanisa moja alipojawa na hasira za mkizi na kumcharaza muumini wa kike kwa kumtumia mumewe arafa ya mapenzi.

Kulingana na mdokezi, mwanamke huyo alikuwa kiongozi wa kwaya ya Kanisa hilo.

Hata hivyo, alikuwa akimmezea mate pasta na majuzi aliamua kumtumia ujumbe katika simu yake akimweleza anavyompenda.

“Mwanamke huyo alikuwa akimtamani pasta wake japo kwa siri. Alishindwa kabisa kumweleza hisia zake hadi majuzi alipoamua kumwandikia ujumbe wa mapenzi,’’ akasema mdokezi.

Inasemekana mke wa pasta alichukua simu ya mumewe kuwasiliana na jamaa zake, aliposikia ujumbe ukiingia kwa simu na akausoma.

Alishangaa kusoma ujumbe huo uliokuwa wa mapenzi.

Alikasirika mno na akamsaka mwanamke huyo ili amfundishe tabia.

“Mke wa pasta aliamua kumsaka mwanamke huyo mitaani ili amfundishe adabu kwa kujaribu kupindua serikali yake. Alimpata katika saluni moja sokoni hapa na ugomvi ukazuka baina yao,’’ akasema mdokezi.

Haki

Inasemekana mke wa pasta alipomuuliza mwanamke huyo sababu ya kumtumia mumewe arafa ya mapenzi, alimpuuza akimwambia alikuwa na haki ya kuwasiliana na yeyote kwa sababu hana mume.

Mke wa pasta alijawa na mori na akamparamia mwanamke huyo mithili ya simba marara.

“Vita viliuma mchanga kati ya mke wa pasta na muumini huyo. Wapita njia walijaribu kuwatenganisha lakini juhudi zao ziliambulia patupu,’’ akasema mdokezi.

Tunaarifiwa kwamba, pasta alipashwa habari kuhusu rabsha hiyo na akafika mara moja na kuwatenganisha.

Hata hivyo, mkewe alianza kumtupia cheche za matusi akimwita mzinifu nambari moja na akatisha kumtaliki.

Kwa bahati, wazee wawili wa kanisa walifika na wakawashauri wakasuluhishe mambo yao nyumbani badala ya kumwaga mtama kwenye kuku wengi.

Dondoo za Hapa na Pale ni visa vinavyojiri kila siku sehemu tofauti nchini na kimataifa. Tuma habari kwa:dondoo@ke.nationmedia.com / taifa@ke.nationmedia.com au swahilihub@ke.nationmedia.com

Share Bookmark Print

Rating