Polo ajuta kudandia lori la polisi usiku

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, January 22  2016 at  17:03

Kwa Muhtasari

Polo wa hapa Kiangoma, Nyeri alilazimika kukesha kwenye seli kwa kudandia lori bila kujua lilikuwa la polisi.

 

KIANGOMA, Nyeri

POLO wa hapa Kiangoma, Nyeri alilazimika kukesha kwenye seli kwa kudandia lori bila kujua lilikuwa la polisi.

Yasemekana jamaa huyo alikuwa amelewa chakari alipotekeleza kitendo hicho.

Kulingana na mdokezi, kalameni ni alikuwa akitoka kwa mama pima kuzima mwasho wa koo lake kwa chang’aa.

Alipofika barabara iliyoelekea mtaa anaoishi jamaa, aliona lori likielekea alikokuwa akienda huku likiendeshwa taratibu.

Bila hata kukagua nambari za usajili, polo alilidandia na kujilaza juu ya mizigo iliyokuwa ndani na kwa sababu ya ulevi alizama kwenye usingizi na kujisahau.

Kulingana na mdokezi, lori hilo lilifululiza mwendo na kituo cha kwanza kusimama kikawa ni kambi ya polisi. Maafisa wa polisi walipoanza kupakua mizigo waliyobeba walipata jombi akikoroma.

“Hei mkubwa uliona uwe miongoni mwa mizigo yetu?” aliuliza afisa mmoja wa polisi akimuamsha.

Kalameni hakuwa na budi ila kutiwa seli hadi siku iliyofuata kwa sababu giza lilikuwa limeingia tayari.

“Jamaa alishtuka kisha akaeleza alivyodandia lori akielekea nyumbani na kuomba msamaha,” akasema mdokezi.

Kufyeka nyasi

Asubuhi iliyofuata, jamaa alipewa adhabu ya kufyeka nyasi kwenye kituo hicho na kuonywa dhidi ya kudandia magari ya polisi.

“Siku nyingine usidandie gari usilolifahamu, hiyo ni kuhatarisha maisha yako kwa sababu hujui watu walilonalo wana nia gani,” alishauriwa na afisa mmoja wa polisi alipoachiliwa huru.

Yasemekana polo alifululiza hadi kwa mama pima na alipohadithia watu kisa hicho waliangua kicheko.

“Jana nimelala seli kama mahabusu kwa kupanda gari la polisi, nitapunguza hii cham na niwe mwangalifu sasa,” alisema polo kila mmoja akimsikiliza na kucheka.

Dondoo za Hapa na Pale ni visa vinavyojiri kila siku sehemu tofauti nchini na kimataifa. Tuma habari kwa:dondoo@ke.nationmedia.com/ taifa@ke.nationmedia.com au swahilihub@ke.nationmedia.com