Polo watwangana kwa sababu ya githeri

Na TOBBIE WEKESA

Imepakiwa - Monday, September 26  2016 at  06:58

Kwa Muhtasari

Makalameni waliokuwa kazini hapa Zimmerman waliwashangaza wapita njia baada ya kupiganana wakizozania githeri.

 

ZIMMERMAN, Nairobi

MAKALAMENI waliokuwa kazini hapa waliwashangaza wapita njia baada ya kupiganana wakizozania githeri.

Makalameni hao ambao ni waashi waliokuwa wakijenga ghorofa moja mtaani humu, walianza kutwangana makonde baadhi walipowamalizia wenzao githeri.

Inasemekana kuwa baadhi ya makalameni walikasirishwa na hatua ya mapolo wenzao kutangulia kwa siri kwa mama mmoja aliyekuwa akiwaandalia chakula na wakala kila kitu.

Duru zinaarifu kuwa mapolo waligundua chakula kilikuwa kimemalizwa na wenzao baada ya kufika kwa mama huyo huku njaa ikiwakeketa.

“Wenzenu wamekuwa hapa wakala kila kitu. Waliniambia kwamba nyinyi leo hampo kazi,” mama aliwaambia mapolo.

Mapolo hao walishangaa jinsi wenzao walivyotoroka kwenda kula bila kuwaarifu.

“Hawa jamaa kwani walikuwa na njama gani? Wanawezaje kutumalizia chakula? Leo watakiona,” polo mmoja aliapa huku akiwaeleza wenzake waende kuwatafuta makalameni.

“Nyinyi mnaezaje kula githeri yote?” polo alimuuliza mwenzake kwa hasira.

Inasemekana kuwa yule jamaa aliyeulizwa alianza kucheka tu. “Sasa unacheka na nani?” polo alimuuliza mwenzake huku akimpa kofi.
Inasemekana wawili hao walianza kutwangana huku wale waliotangulia kula wakimsaidia mwenzao.

Kulingana na mdokezi, makalameni waliokuwa na njaa pia walijiunga na mwenzao kuwapa wenye shibe adabu.

Ujenzi wasitishwa

Duru zinaarifu kuwa shughuli za ujenzi zilisitishwa kwa muda.

“Ukora sisi hatutaki. Ulafi mtaacha,” makalameni waliokosa githeri waliwaeleza wenzao huku wakiwalemea kwa nguvu.

Habari zilizotufikia zinasema iliwabidi wapita njia waingilie kati ili kusuluhisha mgogoro baina ya mapolo.

“Sisi tuliona wamechelewa sana. Tukaamua kwenda kula,” mapolo walianza kujitetea.

Kulingana na mdokezi, ujira wa mapolo wa siku hiyo ulipunguzwa kama njia moja ya kuwapa wote adabu.

Dondoo za Hapa na Pale ni visa vinavyojiri kila siku sehemu tofauti nchini na kimataifa. Tuma habari kwa:dondoo@ke.nationmedia.com / taifa@ke.nationmedia.com au swahilihub@ke.nationmedia.com