Seremala ala makofi kwa kumtamani kidosho

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Tuesday, August 30  2016 at  09:18

Kwa Muhtasari

Kioja kilitokea kwenye matatu moja inayohudumu eneo hili la Wang'uru jombi alipoangushiwa kichapo kikali na buda kwa kukatia mwanadada akiahidi kumfungulia biashara.

 

WANG'URU, Kirinyaga,

KIOJA kilitokea kwenye matatu moja inayohudumu eneo hili la Wang'uru jombi alipoangushiwa kichapo kikali na buda kwa kukatia mwanadada akiahidi kumfungulia biashara.

Minong’ono inaarifu kuwa polo ni seremala mtaani hapa.

Siku ya sinema, kalameni alikuwa akienda kwa mteja wake akiwa amebeba vifaa vyake vya kazi.

Kipusa mmoja aliingia kwenye matatu akiandamana na baba yake ingawa waliketi katika viti tofauti.

“Kidosho aliketi karibu na polo naye baba akaketi nyuma yao,” alisema mdokezi aliyesimulia kuwa jamaa alivunja kimya na kuanza kumrushia kimwana huyo mistari ya mapenzi.

“Madam ninahitaji mke na ninaona Mungu ndiye amekutuma kwangu,” polo alimweleza akimnyoshea mkono wa salamu.

Kipusa hakukataa kumsalimia jombi, alimtazama japo hakusema lolote.

“Ninaelekea kazini na nimebeba vifaa vyangu vya kazi. Nitakufungulia biashara uwe mke wangu,” polo aliendelea kurusha mistari ya mapenzi, akimuonyesha vifaa vyake vya kazi.

Mwanadada asalia kimya

Kalameni aliendelea kuzungumza huku mwanadada huyo akisalia kimya.

Baba wa kidosho aliposikia mazungumzo hayo alimrukia polo na kumuangushia magumi mazito mazito.

“Unasafiri kuenda kazini ama kudanganya wasichana?” alifoka buda akimcharaza kalameni.

“Unadhani kazi unayofanya ndiyo itamlisha binti yangu? Unajua gharama ya kuzaa na kutunza binti kama huyu kweli? Hebu safiri kwa utulivu na uache msichana wangu ama nikuonyeshe kilichomtoa kanga manyonya,” alichemka mzee huyo.

Inasemekana abiria waliingilia kati na kumuokoa polo.

“Pole bwana, umejifunza hufai kumtongoza kila kipusa unayemwona,” alisema mama mmoja na kusababisha watu waangue kicheko.

Penyenye zaarifu kwamba alitulia hadi aliposhuka.